NA BEATUS MAGANJA, MOROGORO
Kamishna mpya wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Ezekiel Mathias Goboro, amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Yussuf Kabange leo Novemba 27, 2026 katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo mkoani Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Goboro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kuiongoza TAWA. Aidha, amewashukuru viongozi na watumishi kwa mapokezi waliyompatia huku akiipongeza menejimenti na watumishi wote kwa jitihada zilizofanywa katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori nchini.
“Ninafahamu kwamba kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika. Kwa matiki hiyo, ujio wangu hapa ni kuongeza nguvu juu ya mafanikio yaliyokwisha kupatikana, kushughulikia kwa pamoja changamoto zilizopo na kuisogeza mbele taasisi yetu,” amesema Kamishna Goboro.
Katika kuimarisha utendaji wa Mamlaka, Kamishna Goboro ameelekeza kuimarishwa kwa usimamizi wa maeneo ya hifadhi, udhibiti wa ujangili, shughuli nyingine haramu pamoja na mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, na kusisitiza uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu, uboreshaji wa huduma kwa wadau na usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, ikiwemo inayohusiana na maandalizi ya AFCON 2027.
Akirejea maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Novemba 25, 2026, Kamishna Goboro amesisitiza kuimarishwa kwa utoaji wa elimu kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kuhusu umuhimu na manufaa ya uhifadhi. Aidha, ameelekeza kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kudhibiti rushwa na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ili kufikia lengo la kukusanya shilingi bilioni 124 katika mwaka wa fedha 2026/2027 na hatimaye Mamlaka kujitegemea kifedha.
Kamishna Goboro amewaomba viongozi na watumishi wote kumpatia ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake, akisisitiza kuwa mafanikio ya TAWA yanategemea umoja, weledi, uadilifu na uwajibikaji wa kila mtumishi. “TAWA ni yetu sote, tushirikiane kuijenga kwa wivu mkubwa,” amesisitiza Kamishna Goboro.
Kwa upande wake, aliyekuwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Yussuf Kabange, amemshukuru Mungu kwa kumpa kibali cha kuiongoza TAWA kwa miaka miwili pamoja na kuwashukuru Makamishna, Maafisa na Askari kwa ushirikiano waliompatia. Ameufananisha uongozi na mbio za kupokezana vijiti ambapo kila mshiriki hukimbia sehemu yake huku wote wakiwa na lengo moja la kupata ushindi.
Aidha, Kabange amewasihi Maafisa na Askari wote wa Mamlaka kumpa ushirikiano wa dhati Kamishna Goboro ili kumwezesha kuiongoza TAWA kwa ufanisi, kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha Mamlaka inafikia malengo yote iliyojiwekea.




Comments