Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemwagiza Waziri wa Kilimo,
Mhe. Daniel Chongolo, kuhakikisha mbolea ya ruzuku inapatikana kwa bei elekezi
ya Serikali katika Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri
ya Wilaya ya Madaba
mkoani Ruvuma, pamoja na maeneo mengine ya mkoa huo, kufuatia malalamiko ya
wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya pembejeo hiyo muhimu.
Makamu wa Rais ametoa agizo hilo,
Novemba 10, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mtyangimbole–Dabaga, wenye thamani
ya shilingi bilioni 5.6, ambao umefikia asilimia 96 ya utekelezaji na
unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 19,000 katika vijiji vitatu.
Katika ziara hiyo, amekagua
matenki ya kuhifadhia maji na miundombinu mingine ya mradi, pamoja na
kuzungumza na wananchi waliopata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili.
Akizungumzia upatikanaji wa
mbolea, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali haiwezi kukubali wananchi
kuuziwa mbolea ya ruzuku kwa bei inayozidi ile iliyoelekezwa, huku akimtaka
Waziri wa Kilimo kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu sababu za kupanda kwa bei
hiyo.
Amesisitiza kuwa bei elekezi ya
Serikali lazima izingatiwe Madaba na maeneo mengine, ili wakulima wanufaike na
ruzuku inayotolewa kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.
Aidha, akizungumzia bei ya mahindi kwa mwaka 2026, Ndejembi amewahimiza wakulima kujiandaa na msimu ujao wa kilimo kwa kuongeza uzalishaji, akieleza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mbolea ya ruzuku inapatikana na changamoto za masoko na bei ya mahindi zinashughulikiwa ili wakulima wasipate hasara.
Kuhusu Mradi wa Maji wa
Mtangimbole–Dabaga, Makamu wa Rais amesema utekelezaji wake ni kielelezo cha
namna Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, inavyoendelea kupeleka huduma muhimu karibu na wananchi na kuboresha
maisha yao.
Amesema Serikali itaendelea
kufanya kazi kwa juhudi ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi mmoja
mmoja, hususan katika maeneo ya vijijini.
Katika hatua nyingine, Makamu wa
Rais amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa
kulinda misitu, kupunguza ukataji miti ovyo na kuhifadhi vyanzo vya maji,
akionya kuwa uharibifu wa mazingira unachangia mabadiliko ya tabianchi, ukame
na kupungua kwa upatikanaji wa maji.
Ziara hiyo imeweka msisitizo
katika dhamira ya Serikali ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo
yanayoonekana, huku changamoto zinazogusa maisha ya wananchi, hususan wakulima,
zikishughulikiwa kwa wakati.




Comments