Kwa unyenyekevu mkubwa, amepokea uhamisho wake kutoka nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Akishukuru Mwenyezi Mungu kwa yote aliyomjaalia yanayoonekana na yasiyoonekana, amemshukuru kwa dhati ya moyo wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kumwamini katika utumishi ndani ya Serikali yake ya Awamu ya Sita. Amesema ni dhamana kubwa na yenye maana kubwa kwake na familia yake.
Asubuhi alipoamka, mwanaye ambaye ni Daktari Tarajali alimuuliza, "Hey, Gentleman, is everything alright?" Akamjibu "very fine", naye akamwambia "Keep it burning" kisha akaenda hospitali kuhudumia wagonjwa.
Amewashukuru wadau wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika majukumu yake ya Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali. Amewashukuru watazamaji, wasikilizaji na wasomaji wote katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambako shughuli zake nyingi zimekuwa huko. Amewashukuru wamiliki wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na akasema waandishi wa habari ni ndugu zake kabisa.
Kama alivyomjibu mwanaye, amesema yuko sawa, yuko tayari kwa kazi na yuko timamu kuitumikia dhamana mpya aliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameomba waendelee kushirikiana katika kulijenga Taifa. "Tuna Tanzania moja tu na sisi ndio Watanzania wenyewe wa kuijenga au kuibomoa. Tuchague kuijenga."
Amewashukuru viongozi na watumishi wote wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali na taasisi zote za Wizara kwa ushirikiano na upendo mkubwa waliokuwa nao, na kuwaomba waendeleze utamaduni huo walioujenga pamoja.
Amewatakia kheri Bw. Abdallah Hassan Mitawi aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Dkt. Ayub Rioba Chacha aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, akisema Mungu awasimamie daima.
Amehitimisha kwa kusema: "Karibuni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum."

Comments