Jana Papa Leo XIV kwa kutumia mamlaka yake ya kitume (kama yalivyoainishwa katika Sheria za Kanisa namba 375 na 377) amefanya mambo makubwa matatu kwa Kanisa la Tanzania;
1). Ameunda Jimbo jipya la Nzega.
2). Amemteua Askofu wa Jimbo jipya la Nzega.
3). Amemteua Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Mwanza.
1). KUUNDWA KWA JIMBO KATOLIKI LA NZEGA.
Papa Leo XIV ameunda rasmi Jimbo jipya la Nzega na hivyo kulifanya kuwa Jimbo la 38 la Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Jimbo hilo jipya litaundwa na wilaya mbili za Nzega na Igunga ambazo hapo awali zilikuwa sehemu ya Jimbo Kuu Katoliki la Tabora. Wilaya nyingine za Mkoa wa Tabora zitaendelea kubaki chini ya Jimbo Kuu la Tabora.
Makao Makuu ya Jimbo hilo yatakuwa mjini Nzega, huku Kanisa Kuu (Cathedral) likiwa ni Parokia ya Mtakatifu Bernadetta iliyopo Nzega mjini.
Jimbo jipya la Nzega lina eneo la kilomita za mraba 14,237, eneo ambalo ni kubwa kidogo kuliko Mkoa wa Kilimanjaro wenye kilomita za mraba 13,250. Kwa mujibu wa takwimu za kichungaji, Jimbo hilo lina jumla ya wakazi 1,263,147 wenye imani mbalimbali. Kati yao, Wakatoliki ni 139,304 sawa na asilimia 11 ya wakazi wote.
Kwa upande wa miundombinu ya kichungaji, Jimbo jipya lina Parokia 13 na Parokia teule 2. Pia lina Mapadre wa Jimbo 25, Mapadre wa Mashirika 8, Shemasi mmoja, Mtawa mmoja wa kiume na Watawa wa kike 66.
Katika sekta za huduma za jamii, Jimbo Katoliki la Nzega lina Hospitali 1, vituo vya afya viwili na zahanati 3. Vilevile lina taasisi 11 za elimu (shule na vyuo).
2). UTEUZI WA ASKOFU WA KWANZA WA JIMBO KATOLIKI LA NZEGA.
Baada ya kuanzisha Jimbo jipya la Nzega kwa kuligawa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Papa Leo XIV amemteua Padre Joseph Mashaka Triphon, C.S.Sp wa Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo hilo jipya.
Kabla ya uteuzi huo, Padre Triphon alikuwa Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria katika Jimbo Katoliki la Bagamoyo.
Askofu mteule Joseph Mashaka Triphon, C.S.Sp alizaliwa tarehe 15 Januari 1962. Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari alipata wito wa upadre na kujiunga na Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (C.S.Sp) kwa ajili ya malezi na mafunzo ya kikasisi.
Kati ya mwaka 1982 na 1984 alipitia hatua za awali za malezi ya shirika. Mwaka 1984 alijiunga na Spiritan Missionary Seminary ya Arusha kwa masomo ya Falsafa na mwaka 1988 alihitimu shahada ya kwanza ya Falsafa (Bachelor Degree in Philosophy).
Mwaka 1989 alijiunga na Chuo Kikuu cha Tangaza jijini Nairobi kwa masomo ya Theolojia na mwaka 1993 alihitimu shahada ya kwanza ya Theolojia (Bachelor Degree in Theology).
Baada ya kuhitimu, alitumwa nchini Papua New Guinea kwa huduma ya kichungaji kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi 1994. Aliporejea aliweka nadhiri zake za kudumu (Perpetual Vows) tarehe 1 Oktoba 1994 na baadaye kupokea Daraja Takatifu la Upadre tarehe 27 Mei 1995.
Baada ya kuwekwa wakfu kuwa Padre, aliteuliwa kuwa Mratibu wa shughuli za kichungaji kwa wanafunzi wa Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (C.S.Sp).
Mwaka 1996 alitumwa nchini Ufaransa katika Chuo Kikuu cha Strasbourg kusomea shahada ya uzamili ya Masuala ya Dini (Master's Degree in Religious Studies) na kuhitimu mwaka 1998. Aliporejea aliendelea na jukumu lake la kuratibu shughuli za kichungaji kwa wanafunzi wa shirika hilo.
Kuanzia mwaka 2003 hadi 2010 alihudumu kama Mweka Hazina (Treasurer) wa Shirika la Wamisionari wa Roho Mtakatifu (C.S.Sp) kwa Kanda ya Afrika Mashariki.
Mwaka 2010 alitumwa tena masomoni nchini Uingereza katika Chuo Kikuu cha Lambeth kusomea Saikolojia na Unasihi (Master of Psychology and Counselling) na kuhitimu mwaka 2012.
Baada ya kurejea Tanzania aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Kipawa. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shule ya Libermann na kuhudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2021.
Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani katika Jimbo Katoliki la Kigoma, ambapo alihudumu hadi mwaka 2025. Mwaka huo huo alihamishiwa kuwa Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria katika Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nafasi aliyokuwa akiitumikia hadi jana alipoteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Nzega.
3). UTEUZI WA ASKOFU MSAIDIZI WA JIMBO KUU KATOLIKI MWANZA.
Papa Leo XIV amemteua Padre Maximilian Francis Buluma kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza. Kabla ya uteuzi huo, Padre Buluma alikuwa Gambera wa kwanza wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Mikaeli, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
Askofu Mteule Maximilian Francis Buluma alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1976 huko Magu, Mkoa wa Mwanza. Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari alipata wito wa upadre na kujiunga na nyumba za malezi ya kikasisi.
Mwaka 1997 alianza masomo ya Falsafa na mwaka 2001 alihitimu shahada ya kwanza ya Falsafa (Bachelor Degree in Philosophy). Baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino Peramiho kwa masomo ya Theolojia na mwaka 2006 alihitimu shahada ya kwanza ya Theolojia (Bachelor Degree in Theology).
Baada ya kukamilisha masomo na malezi yake ya kikasisi, alipokea Daraja Takatifu la Upadre tarehe 10 Desemba 2006. Kisha aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Bernadetta Kahangala hadi mwaka 2007. Baadaye aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Wamisionari ambapo alihudumu kati ya mwaka 2007 na 2008.
Mwaka 2008 alitumwa nchini Italia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thomas wa Akwino kusomea shahada ya uzamili ya Kristolojia (Master's Degree in Christology) na kuhitimu mwaka 2010. Aliporejea nchini aliteuliwa kuwa Katibu Muhtasi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza. Baadaye alitumwa tena nchini Italia kwa masomo ya shahada ya uzamivu ya Kristolojia (PhD in Christology) na kuhitimu mwaka 2015.
Baada ya kurejea alipangiwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Karoli, Ibindo kati ya mwaka 2015 na 2016. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Nyegezi. Mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Mhadhiri wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho na mwaka 2026 aliteuliwa kuwa Gambera wa kwanza wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Mikaeli, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, hadi jana alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.
Tulipongeze Kanisa kwa kuanzisha Jimbo jipya la Nzega na tuwapongeze Maaskofu wapya kwa heshima hiyo kubwa waliyopewa.Tuwaombee na kuwatakia matashi mema wanapoanza majukumu yao mapya ya kulitumikia Kanisa la Mungu.
Roma ikisema, mjadala unafungwa (Roma locuta, causa finita est) 🙏🏽

Comments