NA MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejivunia umahiri ulioonyeshwa na vijana wa Tanzania katika Mashindano ya Olimpiki ya Ujuzi Afrika (African Skills Olympics) yaliyofanyika nchini Algeria, ikieleza kuwa ushiriki huo umethibitisha uwezo wa vijana kushindana katika viwango vya kimataifa.
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa Wizara hiyo, Dkt. Fredrick Salukele, amesema vijana wa Tanzania walioshiriki mashindano hayo wameonyesha uwezo mkubwa, huku wote wakifanikiwa kukamilisha kazi walizopewa ndani ya muda uliopangwa.
Amesema hakuna mshiriki wa Tanzania aliyeshika nafasi za mwisho, jambo linaloonyesha ubora wa mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya elimu ya ufundi na ufundi stadi nchini.
Dkt. Salukele, ambaye pia alikuwa Mwakilishi Rasmi wa Tanzania katika mashindano hayo, ameyasema hayo baada ya kuwasili nchini Novemba 22, 2026, akitokea Algeria akiwa ameambatana na wanafunzi, wakufunzi pamoja na watendaji wa Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Mashindano hayo yalifanyika jijini Oran, Algeria, kuanzia Novemba 16 hadi 20, mwaka huu, yakishirikisha vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Amesema matokeo ya ushiriki huo yanaonyesha kuwa Tanzania ina vijana wenye ujuzi na uwezo wa kushindana kimataifa, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mazingira ya mafunzo kwa kuhakikisha vyuo vinakuwa na vifaa vya kutosha na vya kisasa.
Tanzania iliwakilishwa na vijana watano katika fani za Uchomeleaji (Welding), Upakaji Rangi na Upambaji (Painting and Decorating), Usanifu na Utunzaji wa Mandhari (Landscape Gardening), Uokaji (Bakery) pamoja na Ufundi Bomba na Mifumo ya Joto (Plumbing and Heating).
Dkt. Salukele amesema mashindano hayo yamekuwa fursa kwa vijana kujifunza, kubadilishana uzoefu na washiriki kutoka nchi nyingine na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili mafunzo ya ufundi yaendane na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia.
“Vijana hawa wameonyesha uwezo mkubwa, na sasa ni jukumu lao kutumia ujuzi walioupata kujiajiri au kuajiriwa. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ili vijana waweze kupata ujuzi unaohitajika,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, ambaye alikuwa Mwakilishi wa Kiufundi wa Tanzania, amesema nchi imejifunza umuhimu wa ushiriki wa viwanda na waajiri katika kufanikisha mashindano ya ujuzi kupitia uchangiaji wa vifaa, utaalamu na rasilimali fedha.
Amesema NACTVET inajivunia umahiri wa vijana wanaozalishwa katika vyuo vya kati, akieleza kuwa ujuzi wao ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa Taifa.
Ametoa wito kwa wadau wa sekta ya umma na binafsi kushirikiana katika kuendeleza mashindano ya ujuzi nchini, akibainisha kuwa mashindano hayo yamekuwa changamoto na fursa ya kujifunza kwa taasisi zinazohusika na mafunzo ya ufundi.
Dkt. Lingwanda amesema kuna umuhimu wa kuhakikisha mafunzo yanazingatia maendeleo ya teknolojia ya kisasa na mahitaji ya soko la ajira ili wahitimu waweze kukabiliana na ushindani katika dunia ya sasa.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Bernadetta Ndunguru, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msisitizo katika maendeleo ya viwanda, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi itakayowezesha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya Taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema mafunzo ya ufundi stadi ni sehemu muhimu ya mkakati wa Afrika wa kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi, huku akiwahimiza vijana wanaochagua fani za ufundi kutumia fursa hizo na kupewa maarifa ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, amesema makongamano yaliyofanyika sambamba na mashindano hayo yamekuwa fursa ya mijadala ya kisera kuhusu nafasi ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) katika kuwawezesha vijana kupata ajira, kujiajiri na kukuza ubunifu.
Amesema nchi za Afrika zimekubaliana kuimarisha mifumo na mipango ya utekelezaji wa TVET ili kukuza uchumi wa bara hilo, akieleza kuwa hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema ushiriki wa Tanzania katika mashindano hayo umewapa fursa ya kujifunza mbinu mpya za kuboresha utoaji wa mafunzo na kuimarisha mitaala ili iendane na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Emmanuel Paulo Saimoni, mmoja wa washiriki, amesema mashindano hayo yamempa motisha ya kuendelea kuimarisha ujuzi wake na kumjengea imani kuwa ana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Katika matokeo ya mashindano hayo, Emmanuel Paul wa Chuo cha VETA Dodoma alishika nafasi ya nne kati ya washiriki 12 katika fani ya Usanifu na Utunzaji wa Mandhari, huku Ikwabe Ibrahim wa VETA Dar es Salaam akishika nafasi ya saba kati ya washiriki 26 katika fani ya Upakaji Rangi na Upambaji.



Comments