NDUGAI MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA

Na Mwandishi Wetu
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, ndiye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Jumatatu ya Pasaka Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama alisema Ndugai amethibitisha kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo Dodoma.

Mbali na Ndugai, tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amethibitisha kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

"Napenda kuwaambia kwamba Ndugai amethibitisha kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Dodoma na atashirikiana na Wakristo kusherehekea tamasha hilo kwenye Uwanja wa Jamhuri," alisema Msama.

Msama alimshukuru Ndugai kwa kukubali mwaliko wa kuhudhuria tamasha hilo la Pasaka lililolenga kuchangia watoto yatima na kusaidia wajane wasiojiweza.

Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.

Akizungumza kwa njia ya simu, Ndugai ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, alitoa mwito kwa wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo.

Ndugai alisema Msama Promotions imesaidia vijana, wajane na yatima kupitia tamasha hilo, hivyo ni vizuri kwa wakazi wa Dodoma na Singida kuiunga mkono kampuni hiyo kwa kuingia kwa wingi katika tamasha hilo Jumatatu ya Pasaka.

"Nimefurahishwa na kualikwa kama mgeni rasmi katika tamasha hilo, naamini ndugu zangu wa Dodoma na Singida ni fursa pekee ya kumshukuru Mungu kwa kuwa na tamasha hilo kubwa hapa nchini," alisema Ndugai.

Wasanii wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Rebecca Malope, Rose Muhando, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration, kwaya ya Kinondoni Revival na Mwinjilisti Faraja Ntaboba.

Baadhi ya viongozi waliowahi kuwa wageni rasmi katika matamasha yaliyopita ya Pasaka ni Rais mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi (2000), Mchungaji, Dk. Getrude Rwakatare (2001), Profesa Jumanne Maghembe (2005) aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete.

Wengine ni Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi (2006), Mama Salma Kikwete (2007), Philip Marmo (2008), aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta (2009) na Rais Kikwete (2011). Mwaka 2010 tamasha halikufanyika.

Ciao...

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU