WINGU la rushwa limeendelea kutanda katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa
Mbunge wake wa Ilala, Mussa Zungu, anashilikiwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akituhumiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe
wa Jumuiya ya Wazazi.
Zungu ambaye anakuwa mbunge wa pili wa CCM kunaswa na TAKUKURU kwa tuhuma za
rushwa, anashikiliwa pamoja na wajumbe wawili wa jumuiya hiyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, alikuwa akigombea nafasi ya
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kupitia Jumuiya ya
Wazazi Tanzania Bara na alinaswa juzi sambamba na Dk. Damas Mukasa na Fatuma
Kasenga.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa
Dodoma, Yunis Munisi, alisema Zungu alikamatwa Oktoba 30, mwaka huu, siku moja
kabla ya uchaguzi huo.
Akielezea mazingira ya kukamatwa kwao, alisema Zungu alikamatwa akiwa na
wapambe wake wanne akitoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Kuhusu Dk. Mukasa ambaye alikuwa akigombea nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la
Wazazi Taifa na mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Munisi alisema
alikamatwa Oktoba 8, mwaka huu, nje ya Ukumbi wa Kilimani mjini hapa kwa kosa la
kutoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.
Pamoja na hilo, wajumbe wengine wawili nao wanashikiliwa na TAKUKURU kwa kosa
la kupokea rushwa kutoka kwa Dk. Mukasa ili wamchague.
Mgombea mwingine aliyekamatwa, Fatuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi Mkoa wa Mbeya na Mkutano Mkuu Wazazi Taifa, alikamatwa saa tisa usiku wa
kuamkia jana akiwa analipia baadhi ya wajumbe wa mkutano vyakula na
vinywaji.
“Inaaminika kwamba huo ulikuwa ni ushawishi ili wajumbe
wamchague...alikamatwa katika nyumba ya wageni ya Kitoli iliyopo eneo la Iringa
Road mjini Dodoma,” alisema Munisi.
Alisema TAKUKURU imekuwa ikifuatilia taarifa za vitendo vya rushwa tangu
kuanza kwa chaguzi za ndani za CCM kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo
la kuzuia na kupambana na vitendo hivyo.
Munisi alisema hatua hiyo imefanikiwa kuzuia vitendo vingi ambavyo vilitaka
kutendeka baada ya kupata mipango hiyo na kuitibua kabla ya kufanikiwa.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni kitendo cha
wajumbe kushirikiana na wagombea na wapambe wao katika vitendo vya rushwa, na
hivyo kuwa shida kufanya ushirikiano.
Alisema changamoto nyingine inatokana na wananchi kudai wameona vitendo vya
rushwa vikitendeka, lakini hawachukui hatua zozote za kutoa taarifa
TAKUKURU.
Kuhusu tuhuma zinazowakabili akina Zungu na wenzake, alisema uchunguzi
unaendelea.
Kambi ya Lowassa kidedea
Kambi inayoungwa mkono na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imezidi
kuonesha umwamba wake ndani ya CCM kwa kuibuka kidedea katika uchaguzi wa
Jumuiya ya Wazazi uliofanyika jana.
Abdallah Bulembo ndiye ameibuka mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya
hiyo kwa kura 677 na kuwatimulia vumbi washindani wake, Martha Mlata aliyepata
kura 146 na John Barongo aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kuambulia kura 43.
Mapema akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib
Bilal, aliitaka jumuiya hiyo kuchagua viongozi watakaoweza kukiepusha chama na
rushwa kwa kipindi chao cha miaka mitano.
“Kiongozi anayehonga ili aweze kupata madaraka huyo si kiongozi na hafahi
kuchaguliwa,” alisema Dk. Bilal na kuwataka wagombea wote kuachana na imani ya
kutumia fedha kutafuta uongozi.
Aidha, makamu huyo aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuwalea
vijana ili maadili yaliyopotea yarudi kama hapo awali.
Dk. Bilal alisema kuwa wazazi ndio wenye jukumu kubwa la kuwalea vijana na
kuwaongoza katika maadili mema, hivyo ni jukumu lao kubwa kuhakikisha vijana
wanakuwa na tabia njema.
|
Comments