BUNGE LAPITISHA TRILIONI 2.5 KWA WIZARA YA UJENZI.

📌BARABARA NA MADARAJA KUNUFAIKA ZAIDI


Bunge limepitisha kwa kishindo Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na taasisi zake ya Sh trilioni 2.564 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo kati ya fedha hizo Sh trilioni 2.467 sawa na asilimia 97 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo barabara na madaraja.



Kati ya fedha za maendeleo, kiasi cha Sh. Trilioni 1.545 ni fedha za ndani, ambapo Sh. Trilioni 1.047 zimetengwa kupitia Mfuko wa Barabara na Sh. Bilioni 497.47 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, huku Sh. Bilioni 922.46 zikiwa ni fedha za nje.



Kupitia bajeti hiyo, Wizara inatarajia kujenga barabara na madaraja nchi nzima ili kuendana na kasi ya ufanisi wa bandari pamoja na ukuaji wa shughuli za viwanda, kilimo, utalii na sekta nyingine za uchumi.


Katika utekelezaji wa bajeti hiyo, vipaumbele vya Wizara vitaweza kuifungua nchi kwa kumaliza kero za miundombinu ya barabara na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi.


Pia, Serikali inalenga kujenga msingi wa miundombinu ya kisasa, imara na yenye uwezo wa kuhimili changamoto zinazotokana na ongezeko la mahitaji ya miundombinu.


Wizara pia itaelekeza nguvu katika ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano wa magari katika majiji na miji, ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, Tanzania na nchi jirani pamoja na maeneo ya kimkakati ya kiuchumi.


Aidha, ujenzi wa barabara zinazoelekea katika maeneo ya kimkakati kama bandari, reli, viwanja vya ndege, viwanda, miji mikuu na maeneo ya ulinzi wa mipaka utaendelea sambamba na ukarabati wa maeneo yenye changamoto katika barabara kuu na za mikoa.


Kupitia bajeti hiyo pia, Wizara itaendelea kuimarisha usafiri na miundombinu ya vivuko, kuwajengea uwezo wataalamu na wakandarasi wa ndani katika sekta ya ujenzi pamoja na kuendelea na ujenzi wa majengo ya Serikali na nyumba za gharama nafuu.


“Waheshimiwa wabunge tunaomba mtuamini, mtutume kazi na tumejipanga kwenda kufanya kazi,” amesema Waziri Ulega.



 


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

Kizza Besigye ‘akamatwa’ tena Uganda

Wasifu wa Kizza Besigye

TANZIA;.KWA KHERI DADA YETU MPENDWA EDITHA, TASNIA IMEPATA PIGO

IJUE HISTORIA YA PACOME ZOUZOUA

NATAKA TANZANIA, KENYE NA UGANDA IWE NCHI MOJA, ILI BAHARI YA HINDI IWE YETU SOTE - MUEVENI

RAIS SAMIA AWASILI IRINGA KWENDA MEI MOSI NJOMBE