Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Modesta Nyagawa akimpima kiwango cha sukari kwenye damu mkazi wa Njombe aliyefika katika Hoteli ya Agreement iliyopo mjini Njombe kwaajili ya kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zinayotolewa kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kilichoandaliwa na Idara ya Habari- Maelezo.
**********************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imewahimiza wananchi
kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara kupitia kampeni ya “Jua
Namba Zako” ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa ya moyo na
kupata matibabu kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa Taasisi hiyo Samweli
Mbilinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za upimaji wa
moyo zinazotolewa na JKCI kwenye Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari,
Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kinachofanyika katika Hoteli ya
Agreement iliyopo mjini Njombe.
Dkt. Mbilinyi alisema wananchi wengi bado hawana uelewa wa
kutosha kuhusu magonjwa ya moyo jambo linalosababisha baadhi yao kuishi na
matatizo hayo bila kujitambua hadi wanapofika hospitalini wakiwa na matatizo
mengine.
Alitoa mfano wa mgonjwa aliyefika katika upimaji huo ambao
huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali zinatolewa kwajili ya matatizo ya
miguu lakini baada ya kupimwa alibainika kuwa na shinikizo kubwa la damu
lililozidi kiwango cha kawaida hali iliyowalazimu wataalamu wa JKCI kumfanyia
vipimo vya moyo na kuanza matibabu mara moja.
“Tumegundua wananchi wengi hawajawahi kupima afya ya moyo
wala kufahamu viwango vyao vya afya. Kupitia kampeni ya Jua Namba Zako tunawahamasisha
wananchi wajitokeze kupima ili kujua hali zao mapema na kupata tiba stahiki”,
alisema Dkt. Mbilinyi.
Dkt. Mbilinyi alisema katika upimaji unaoendelea wamebaini
watu wengi wenye shinikizo la juu la damu na matatizo ya moyo ambao hawakuwahi
kufanyiwa vipimo vya moyo wala kujua hali zao za afya.
Aliishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
kwa kuwezesha upatikanaji wa dawa bure kwa wananchi wanaobainika kuwa na
matatizo mbalimbali ya afya ikiwemo magonjwa ya moyo katika upimaji huo.
“Ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya zao.
Watakaobainika kuwa na changamoto watapatiwa ushauri wa kitaalamu, tiba, dawa
bila malipo na rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI”, alisisitiza.
Kwa upande wao wananchi waliopata huduma hizo walieleza
kufurahishwa na ujio wa wataalamu wa JKCI mkoani Njombe huku wakisema
umewasaidia kupata huduma karibu na maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri
kwenda Dar es Salaam.
Mmoja wa wananchi hao Farida Fredrick kutoka kijiji cha
Ihalula, alisema alifika kupata huduma baada ya kusikia madaktari wa JKCI
wanatoa huduma Njombe.
“Mimi ni mgonjwa wa moyo na huwa nahudhuria kliniki ya JKCI
Dar es Salaam. Niliposikia madaktari wako hapa Njombe nikaona nitumie nafasi
hii kupata huduma karibu na nyumbani, huduma ni nzuri sana na wananchi wengi
wajitokeze kupima”, alisema Farida.
Joseph Mwakalonge mkazi wa Njombe mjini alisema alikuwa
akisumbuliwa na maumivu ya kichwa pamoja na uchovu wa mara kwa mara bila
kufahamu chanzo chake lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na
shinikizo la juu la damu na kupewa matibabu.
“Naishukuru sana JKCI kwa kuleta huduma hizi karibu yetu.
Sikuwahi kujua kama nina tatizo la presha kubwa kiasi hiki lakini leo nimepata
elimu, vipimo na dawa kitu ambacho kitanisaidia kuutunza moyo wangu mapema ili
usipate madhara zaidi”,alisema Mwakalobe.
Naye Rehema Mlowe mkazi wa Makambako alisema alikuwa
hajawahi kupima afya ya moyo tangu alipogundulika kuwa na changamoto ya presha
miaka miwili iliyopita lakini ujio wa madaktari wa JKCI umempa nafasi ya
kufanyiwa uchunguzi wa kina na kupata ushauri wa namna ya kuishi kwa kufuata
mtindo bora wa maisha.
“Nimepata huduma nzuri na wataalamu wanatoa elimu kwa upendo
mkubwa. Ninawaomba wananchi wenzangu watumie fursa hii kuja kupima afya zao
mapema kabla hali haijawa mbaya”, alisema Rehema.
Katika upimaji huo JKCI inatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, uchunguzi wa shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia uwingi wa sukari kwenye damu, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, elimu ya lishe bora na mtindo sahihi wa maisha, elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa moyo.




Comments