WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA MATOKEO YA TAFITI ZA: UWEZESHAJI WA WANAWAKE NA LISHE PAMOJA NA TAFITI YA JINSIA NA MAZINGIRA*
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, *Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,* leo Mei 6, 2026, jijini Dodoma, amezindua rasmi matokeo ya tafiti mbili: Uwezeshaji wa Wanawake na Lishe (2023/24) pamoja na Jinsia na Mazingira (2025), akisisitiza haja ya kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za usawa wa kijinsia, lishe na mazingira.
Amesema tafiti hizo zinaonesha kuwa ni asilimia 26 tu ya wanawake wanaoamini wana uhuru wa kufanya maamuzi ya kiuchumi, huku asilimia 34.1 wakikubali kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ndoa, talaka na uzazi, na asilimia 54.6 wakikataa aina zote za ukatili wa kijinsia.
*Dkt. Gwajima* amesema bado kuna pengo kubwa katika maamuzi ya kifedha, ambapo wanaume wanaongoza kwa asilimia 54.8 dhidi ya wanawake asilimia 39.6. Hata hivyo, wanawake wana ushawishi mkubwa zaidi katika matumizi ya muda (asilimia 43.3) ikilinganishwa na wanaume (asilimia 39.4).
Katika eneo la rasilimali na lishe, ameeleza kuwa asilimia 58 ya wanawake wanatumia huduma za kifedha ikilinganishwa na asilimia 72 ya wanaume, huku asilimia 40 wakimiliki mali, lakini wachache wakiwa na umiliki rasmi. Kwa upande wa lishe, asilimia 56.7 ya wanawake wanakidhi kiwango cha chini cha lishe bora, huku baadhi ya maeneo ya vijijini yakishuka hadi asilimia 39 kutokana na upatikanaji mdogo wa vyakula muhimu.
Akihitimisha, *Dkt. Gwajima* amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kupitia upatikanaji wa mikopo, elimu ya kifedha na umiliki wa mali, pamoja na kuongeza ushiriki wao katika maamuzi na nafasi za uongozi. Aidha, juhudi zitaelekezwa katika kuhamasisha lishe bora, kuimarisha matumizi ya takwimu katika mipango ya maendeleo, na kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika masuala ya mazingira ili kujenga jamii yenye ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, *Dkt. Amina Msengwa,* amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika uzalishaji wa takwimu sahihi na za kuaminika, huku akisisitiza umuhimu wa kuzisambaza ili zitumike ipasavyo katika kupanga sera na mipango ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Takwimu na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania *Mhe. Anne Makinda,* ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi kutumia kikamilifu takwimu hizo katika kufanya maamuzi sahihi, akisisitiza kuwa uwekezaji katika takwimu bora ni msingi wa maendeleo endelevu.



Comments