Na Mwandishi wetu - MichuziTv
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameielekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara katika vyama vya ushirika nchini ili kudhibiti ubadhirifu wa mali, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha vyama hivyo vinatoa huduma bora kwa wanachama wake.
Dkt. Nchimbi amesema Serikali imejipanga kuifanya sekta ya ushirika kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa kwa kuhakikisha mali za vyama vya ushirika zinalindwa, zinasimamiwa kwa ufanisi na zinatumika kwa manufaa ya wakulima na wanachama wote.
Amesema ukaguzi wa mara kwa mara utasaidia kubaini mapema changamoto zinazojitokeza katika vyama vya ushirika, hivyo kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa kabla ya kusababisha hasara au matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za wanachama.
Aidha, Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha vyama vya ushirika kuimarika zaidi ili viweze kuongeza mchango wake katika kuinua uzalishaji wa kilimo, kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Ameeleza kuwa kwa sasa Tanzania ina vyama vya ushirika 2,531 ambavyo vinaendelea kuwa daraja muhimu la kuwafikishia wananchi huduma mbalimbali, hususan katika sekta ya kilimo, na kusisitiza kuwa vinapaswa kuendelea kuimarishwa ili viendane na mahitaji ya maendeleo ya nchi.
"Vyama vya ushirika vina nafasi kubwa katika maendeleo ya wananchi. Tunapaswa kuviwezesha na kuviimarisha ili viweze kutoa huduma bora zaidi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi," amesema Dkt. Nchimbi.
Pia amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo, akibainisha kuwa thamani ya biashara iliyofanywa kupitia vyama vya ushirika imeongezeka kutoka Sh trilioni 4.2 hadi kufikia Sh trilioni 4.9 katika msimu wa mwaka 2025/2026.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa mitaji ni msingi muhimu wa kuimarisha uwekezaji katika sekta ya kilimo, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata fursa za kifedha zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao yao.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika, Benson Ndiege, amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeanzisha mfumo maalumu wa kutambua na kuhakiki mali zinazomilikiwa na vyama vya ushirika nchini kwa lengo la kuwa na taarifa sahihi zitakazorahisisha usimamizi na matumizi yake.
Amesema mfumo huo utawezesha kujua thamani halisi ya mali za vyama vya ushirika, kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na kuongeza uwazi katika usimamizi wa rasilimali za vyama hivyo.
Ndiege amesema hadi sasa mali 5,558 za vyama vya ushirika zimetambuliwa na kufanyiwa tathmini, zikiwa na thamani ya Sh milioni 18.6, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea sambamba na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za ushirika zinafuatwa.
Aidha, ametoa wito kwa wanachama na wadau wa sekta ya ushirika kushirikiana na Tume kwa kutoa taarifa na ushirikiano utakaosaidia kulinda mali za vyama hivyo na kuimarisha utendaji wake.
Naye Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo, amesema Serikali itaendelea kuifanya sekta ya ushirika kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa misingi ya uwazi, ufanisi na uwajibikaji.
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)


Comments