KUTOKA milima ya Uluguru mkoani Morogoro hadi Cambodia, panya Magawa ameacha historia ya aina yake baada ya kufundishwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na shirika la APOPO, kisha kusaidia kugundua mabomu ya ardhini na kusafisha maelfu ya mita za mraba za ardhi iliyokuwa hatarishi.
Kutokana na mchango wake mkubwa katika kuokoa maisha ya watu, Magawa sasa anaendelea kuishi katika kumbukumbu za wananchi wa Cambodia, ambako amejengewa mnara wa kumbukumbu katika mji wa Siem Reap.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Agosti 31, 2026, Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, amesema historia ya Magawa ni ushahidi wa uwezo wa Tanzania katika kutumia utafiti na wanyama wa asili kutatua changamoto zinazowakabili binadamu.
Amesema panya wanaotumika katika mradi huo ni panya wa asili wa Tanzania, waliokamatwa awali katika milima ya Uluguru, Morogoro, na ambao sasa wanaendelea kuzalishwa na kufundishwa katika kituo maalumu cha SUA.
“Panya wanazaliwa, wanafundishwa hadi kustaafu”
Profesa Chibunda amesema SUA imeweka mfumo maalumu wa kuwahudumia panya hao katika kila hatua ya maisha yao, kuanzia kuzaliwa, mafunzo, kufanya kazi hadi kustaafu.
“Ukija pale kwetu utakuta tuna wodi ya wazazi, tuna wale ambao wanaanza mafunzo, kuna waliohitimu mafunzo, lakini vilevile tuna banda ambalo ni la panya wastaafu. Wako pale wanapata pensheni,” amesema.
Amesema Tanzania haina changamoto kubwa ya mabomu ya ardhini, hivyo wataalamu wa mradi huo hushirikiana na nchi ambazo bado zinakabiliwa na tatizo hilo.
Kwa mujibu wake, Cambodia ni miongoni mwa nchi hizo kutokana na historia ya migogoro iliyosababisha kuwepo kwa mabomu mengi yaliyosalia ardhini.
Magawa avunja rekodi Cambodia
Profesa Chibunda amesema Magawa alipelekwa Cambodia na kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa, akivunja rekodi kwa kugundua mabomu mengi zaidi kuliko panya wengine waliowahi kutumika katika kazi hiyo.
Magawa alifanya kazi nchini humo kuanzia mwaka 2016 hadi alipostaafu mwaka 2021, ambapo alifanikiwa kugundua zaidi ya mabomu 100 ya ardhini na mabaki ya vilipuzi, huku akisaidia kusafisha zaidi ya mita za mraba 141,000 za ardhi, eneo linalokadiriwa kuwa sawa na takribani viwanja 20 vya mpira wa miguu.
Kutokana na mafanikio hayo, Magawa alitambuliwa kimataifa na kutunukiwa Medali ya Dhahabu ya PDSA, heshima inayotolewa kwa wanyama walioonyesha ujasiri na kutoa mchango mkubwa katika huduma kwa binadamu.
Magawa ageuka shujaa, ajengewa mnara
Profesa Chibunda amesema Magawa alifikia umri wa uzee baada ya kutumikia kwa miaka kadhaa, na baadaye alifariki.
“Panya wale umri wao ni miaka minane. Akifika tisa ni mzee kweli hata hana meno. Kwa hiyo Magawa umri wake ukafika na bahati mbaya akafariki,” amesema.
Amesema baada ya kifo chake, kulikuwa na mpango wa kumrudisha Tanzania kwa ajili ya mazishi, lakini haukuweza kutekelezwa kutokana na changamoto za vibali na taratibu za usafirishaji.
Badala yake, amesema Cambodia iliamua kumuenzi kwa kumjengea mnara mkubwa katika mji wa Siem Reap.
Mnara huo wenye urefu wa takribani mita 2.2 ulizinduliwa Aprili 3, 2026, ukiwa unaonesha Magawa akiwa amevaa medali yake, huku chini yake kukiwa na mfano wa bomu la ardhini na mabaki ya vilipuzi alivyosaidia kuvigundua.
“Lakini wamemjengea mnara mkubwa kule, na sisi ukija chuoni kwetu tuna barabara mahsusi inaitwa Barabara ya Magawa,” amesema Profesa Chibunda.

Comments