Mwenyekiti wa UWT CCM Taifa, Mary Chatanda
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. KAZI IENDELEE.
Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa nanyi viongozi wenzangu wa UWT kwa itifaki nilizowataja. Nawapongeza sana kwa kazi mbalimbali zinazoendelea katika maeneo yenu maana nawaona katika mitandao mbalimbali Hakika UWT ni moto moto hongereni sana .
Leo tumekutana hapa ili kutoa maelekezo ya namna ya kusherekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya familia inayofanyika kila tarehe 15/5 .
Ndugu Viongozi wa UWT na wanahabari Kabla sijaendelea napenda kwanza niendelee kumpongeza Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa namna ambayo ameimarisha misingi ya Demokrasia ya Vyama vingi kupitia mfumo anaotumia kuongoza Nchi kwa maana Maridhiano ,Ustahamilivu , Mageuzi na Ujenzi mpya maarufu Four R ambao umewezesha kuwa na maridhiano na vyama vya Siasa .Kwenye mkutano baina ya Mhe Rais DK Samia Suluhu Hassan ambae ni Mwenyekiti wa Chama chetu cha CCM na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu uliofanyika tarehe 3/1/2023 aliruhusu Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa , alitangaza utayari wa Serikali kukwamua mchakato wa Katiba mpya , pia alitoa taarifa ya dhamira ya serikali anayoiongoza kuzifanyia kazi sheria mbalimbali zinazohusu uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa .
Ndugu Viongozi wa UWT na wanahabari tangu wakati huo tumeshuhudia Vyama mbalimbali vya Siasa vyenye usajili wa kudumu vikiendelea na shughuli mbalimbali za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara ,mikutano ya ndani katika maeneo mbalimbali Nchini bila bugudha ya aina yoyote si tu kwa vyama peke yake bali pia sisi wanawake kupitia jumuiya zetu ndani ya vyama tumekuwa na wakati mzuri wa kufanya siasa katika mazingira ya maridhiano yaliyotengenezwa na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan .
Mnamo tarehe 11/5/2023 Baraza la Wanawake Chadema lilifanya maandamano ya amani ya kumtaka Mhe Spika awaondoe Bungeni Wabunge wa Viti Maalum 19 kupitia CHADEMA kwa hoja kuwa si wanachama wao . Siko hapa kupinga maandamano hayo lakini nipo hapa kutoa masikitiko yangu kwa niaba ya UWT na wanawake wengine kutokana na baadhi ya kauli na mabango yenye ujumbe uliomuhusisha moja kwa moja Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambazo zilikuwa si za kiungwana na kebehi kwa kiongozi wa Nchi .
Moja ya Bango lilikuwa na Ujumbe huu “SAMIA TULIKUKARIBISHA MOSHI KWA HESHIMA WEWE UMETULIPA DHARAU ” kwanza niweke wazi kuwa BAWACHA ndio waliomuomba Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani 8/3/2023 , wao ndio walimuhitaji sana Mhe Rais kwenye Maadhimisho hayo kuliko yeye alivyowahitaji
Sisi UWT tunaendelea kumpongeza Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mwaliko wa BAWACHA na kupitia utayari wake huo Duniani ilishuhudia kitendo chake cha kiungwana ambacho hakijawahi kufanyika si tu hapa Nchini bali Duniani wa kiongozi wa juu wa Serikali wa Chama kinachotawala kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi kutoka Chama Cha Upinzani lakini Mwanamke shupavu ,rahimu ,msikivu na mkarimu Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan alikubali mwaliko huo na hivyo kuonyesha kwa vitendo kuwa amedhamiria kuliunganisha Taifa na kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti za kiitikadi .BAWACHA inapaswa kuendelea kuheshimu na kuenzi uamuzi wa Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan wa kukubali mwaliko na kujumuika nao jambo ambalo pia liliipa heshima na hadhi kubwa maadhimisho hayo kuliko wakati wowote waliowahi kuandaa maadhimisho ya aina hiyo .
Katika Maadhimisho hayo BAWACHA waliwasilisha jambo lao la kutaka Wabunge wao waondolewe Bungeni , Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliwaeleza wazi kuwa hilo jambo lipo Mahakamani na hivyo usubiriwe uamuzi wa Mahakama . Maelezo haya ya Mhe Rais Samia yanaonyesha ni kwa namna gani utawala wake unazingatia Sheria na Katiba ya Nchi na kwamba Mahakama ni Chombo huru hakipaswi kuiingiliwa .
Kitendo cha BAWACHA kutumia hoja ya kuwaondoa Wabunge wao 19 Bungeni wakimuhusisha Mhe Rais DK Samia tena kwa kutumia lugha ya kejeli bila kuheshimu mamlaka yake na pia kutumia tu Jina lake moja Samia si cha kiungwana kabisa na hakiendani na Heshima aliyowapa ya kukubali mwaliko wao wa 8/3/2023 na mil ana desturi zetu za kuheshimu viongozi wetu n ahata wale waliotuzidi kiumri .
Ndugu Viongozi wa UWT na wanahabari mtakumbuka kuwa baada ya Mkutano wa CHADEMA sisi UWT tuliandaa Mkutano mkubwa wa Uwanja wa Uhuru DSM 19/3/2023 kumpongeza Mhe Rais Dk Samia kwa kutimiza miaka miwili madarakani ambao ulihudhuriwa na Wanawake kutoka sehemu mbalimbali za Nchi hii takrbani wanawake wasiopunga 15,000 wakiwemo wanawake wa vyama vingine vya siasa ni wazi kuwa mkutano huo ulimpa heshima zaidi Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuliko Mkutano wa BAWACHA Moshi .Kwa makuzi yake na kwa aina ya uongozi wa Mhe Rais Samia hajawahi kuonyesha dharau ya aina yoyote amekuwa mtu muungwana ,rahimu ,msikivu ,mstahamilivu,msamehevu na mwenye upendo kwa wananchi wake anaowaongoza bila ya kujali dini ,rangi,kabila na tofauti za kiitikadi
Ndugu Viongozi na wanahabari ,Maelezo yaliyotolewa na Catherine Ruge Katibu wa BAWACHA alipoulizwa na Muandishi juu ya Tafsiri ya maneno “SAMIA TULIKUKARIBISHA MOSHI KWA HESHIMA WEWE UMETULIPA DHARAU ” kwmba Rais Samia ni Mlipaji Mkuu , ndio mwajiri akiacha kuwalipa Wabunge hao 19 hawatakuwepo kauli hii sio sahihi kabisa kwani kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2001 kifungu 6(7) Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ndio Mlipaji Mkuu wa Serikali na sio Mhe Rais , na pia Mwajiri wa Wabunge wakiwemo Wabunge wa Viti Maalum wanaopatikana kwa mujibu wa ibara 66(b) sio Mhe Rais .
Ndugu Viongozi wa UWT na wanahabari naomba niwatake Viongozi wa BAWACHA na wanachama wao warejee ibara 107A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayosema nanukuu “Mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa idara ya Mahakama na idara ya Mahakama ya Zanzibar , na kwahiyo hakuna chombo cha Serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki” .Hivyo si Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan wala Mhe Spika Dk Tulia Ackson wenye mamlaka ya kuwaondoa Wabunge hao Bungeni na tunawataka kuacha mara moja upotoshaji wa aina hii .
Kuendelea kufanya maandamano na kutoa kauli za kebehi kwa Mhe Rais na kwa Mhe Spika haitawasaidia bali waichie Mahakama ikamilishe kazi yake na kutoa uamuzi wake juu ya Maombi ya Wabunge wao 19 ambao wametumia haki yao kikatiba kwenda Mahakama Kuu kwa shauri lao la kupinga kufukuzwa Uanachama . kwa kufanya hivyo watakuwa wanaheshimu mhimili wa Mahakama ambalo ni jambo muhimu sana kwa Chama kinachojinasibu kwamba kina nguvu na kipo tayari kushika dola . BAWACHA wanayofursa nao kutumia chombo cha Mahakama kupinga wabunge hao kuendelea kuwa wabunge wakati huu wana kesi mahakamani kuliko hivyo wanavyofanya kutumia janja janja waonekana wana hoja .
Ndugu Viongozi wenzangu na wanahabari ,UWT inaheshimu maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa mpaka sasa na uhuru wa kuendesha shughuli mbalimbali za kisiasa na uhuru wa kujieleza ambao unalindwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata ukosoaji kwa Serikali yetu hata hivyo haitakuwa tayari kuvumilia uhuru huo kutumika vibaya mfano lugha ya matusi , udhalilishaji na wenye kutweza utu na hasa ukiwa unamlenga Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan na pia Mkuu wa Mhimili wa Bunge Mhe Spika Dk Tulia Ackson .
Uwt hatutavumilia katika hili tutasimama imara ili kudumisha misingi ya kuheshimiana hasa katika wakati huu wa kujenga demokrasia imara na Utawala wa sheria . Tunampongeza sana Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo Msajili wa Vyama vya Siasa ya kuanza rasmi kwa Mchakato wa Katiba mpya na dhamira hii imeonekana moja kwa moja kwenye wasilisho la Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria .
Ndugu Viongozi wa UWT na wanahabari Kulekea maadimisho ya Siku ya Familia Kimataifa 15/5/2023 yenye KAULI MBIU “IMARISHA MAADILI NA UPENDO KWA FAMILIA IMARA ”napenda kutoa maelekezo kwa UWT ngazi zote Tawi ,Kata ,Wilaya ,Mkoa kufanya makongamo mbalimbali ya kuwaleta wanawake pamoja na kuelimisha kuhusu Maadili na kupiga vita mmonyoko wa maadili ndani ya Nchi yetu . Nasisitiza kuendelea kumuunga mkono Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwenye moja ya ajenda anayosimamia kwa karibu inayohusu ujenzi wa kizazi chenye maadili kwa kutekeleza yote aliyoagiza kwa nyakati mbalimbali ikiwemo kupitia hotuba yake ya hivi karibuni kwenye Baraza la Eid Fitri lililofanyika Dar-Es-Salaam 22/4/2023 .
UWT tutumie Siku ya Familia Kimataifa kuhimiza umuhimu wa Familia hasa wazazi kutoa malezi stahiki na uangalizi wa familia hasa watoto wadogo wakike na wakiume ili kuwalinda dhidi ya matukio ya ukatili . Pia tuhimize upendo ndani ya familia ili kuweza kujenga familia bora na kupunguza kabisa matukio ya ukatili ndani ya familia ikiwemo matukio ya mauaji Tutakapojenga Familia Imara ndio Taifa imara pia .
Ndugu Viongozi wenzangu na wanahabari Hivi karibuni UWT Taifa tutoa taarifa ya matokeo ya ziara zilizofanywa na ngazi za wilaya mpaka mkoa kutembelea madawati ya Jinsia katika vituo vya Polisi wakati wa maazimisho ya siku ya Mwanamke Duniani iliyofanyika 8/3/2023 ili kupata taarifa za matukio hayo na hatua zilizochukuliwa pamoja na mikakati endelevu ya kupambana na ukatili huu kwa wanawake na watoto pamoja na kukemea vitendo kinyume na maadili yetu ikiwemo Ndoa za Jinsia moja . Nawapongeza sana kwa ziara zinazoendelea mashuleni Nchi nzima kuelemisha watoto juu ya vitendo vya kikatili dhidi yao .
Wajibu huu tunaofanya sasa UWT ni moja ya maelekezo yaliyotolewa na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kumi wa Uchaguzi wa UWT Taifa tarehe 28/11/2022 Hakika UWT imeanza safari hakuna kurudi nyuma .Tanzania ya Rais Samia bila matukio mengi ya ukatili wa kijinsia inawezekana .
Napenda kuchukua fursa hii kuwatakia wanawake wote Maadhimisho mema ya Siku ya Familia ,tukumbuke kuwa sisi Wanawake ni chachu katika kujenga Familia imara yenye Maadili na upendo endapo tutatimiza wajibu wetu kwa kuwa Mama ni Mlezi kwa asili yake . UWT inamtakia heri Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika majukumu yake na tunamuunga mkono kwenye kazi yake njema inayoendelea ya kuiletea Nchi maendeleo katika Sekta zote .
Ahsanteni kwa kunisikiliza
UWT IMARA ,JESHI LA MAMA, KAZI IENDELEE
MCC Mary Pius Chatanda,
Mwenyekiti wa UWT Taifa,
MEI 12 ,2023

Comments