Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Brazil kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 utakaofanyika tarehe 18-19 Novemba 2024 jijini Rio de Janeiro.
Taarifa hii iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inasema, Rais Dkt. Samia amealikwa na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil, Mhe. Luiz Inácio Lula da Silva na Mwenyekiti wa G20 kushiriki mkutano wa jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimataifa kwenye masuala ya kiuchumi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuhudhuria katika mkutano wa G.20. Mwaliko huu unatokana na heshima na ushawishi mkubwa ambao Rais Dkt. Samia amejijengea kwenye majukwaa ya kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo Rais Dkt. Samia anatarajia kushiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa na umasikini, kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.
Rais Dkt. Samia anatarajia kutumia jukwaa hilo linalokutanisha nchi zenye chumi kubwa zaidi duniani kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kujenga maendeleo endelevu na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowaletea ustawi Watanzania kupitia sekta za uzalishaji.
Akiwa nchini Brazil, Rais Dkt. Samia atafanya mikutano ya pembezoni na taasisi kubwa za kifedha duniani pamoja na kukutana kwa mazungumzo na Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na baadhi ya nchi wanachama wa G.20 akiwemo mwenyeji wake Brazil.
Aidha, lengo la mazungumzo hayo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya uwili hususan kwenye sekta ya viwanda, biashara, kilimo, nishati utalii pamoja na kutafuta fursa mbalimbali za ushirikiano, uwekezaji na miradi ya pamoja.
Ushiriki wa Rais Dkt Samia kwenye Mkutano wa G20 unalenga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuchangia ipasavyo mijadala muhimu ya kimataifa kuhusu maendeleo duniani na kunadi sera za uchumi za kimataifa zitakazochochea maendeleo na ustawi zaidi nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Comments