NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imekiri kuvutiwa na mchango mkubwa wa Benki ya NMB kwa makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kusaidia utatuzi wa changamoto za Watoto Yatima na Wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu, iliyoutaja kuwa ndio siri ya mafanikio yaliyotukuka ya benki hiyo inayopata siku baada ya siku.
Hayo yamesemwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Zubeir Ali Maulid, kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, wakati wa Hafla ya Iftar iliyoandaliwa na NMB kwa ajili ya wateja wao, viongozi wa Serikali, wa dini na Watoto Yatima na Wanaoishi Mazingira Magumu Zanzibar.
Iftar hiyo iliyofanyika Jumatano Machi 12 mjini Unguja, ilijumuisha takribani watoto 70 kati ya 106 wanaolelewa na Kidundo Orphanage (30) na Muftuh Foundation (76) vya Zanzibar, ambapo NMB iliwakabidhi misaada mbalimbali ya vyakula na kuweka ahadi ya kuwahudumia watoto hao katika mwezi mzima wa Ramadhani.
Kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Spika Maulid aliishukuru NMB kwa kujali makundi mbalimbali ya kijamii, hususani ya Watoto Wenye Uhitaji na kwamba moyo wa kutoa na kuthamini vijana hao, umesaidia kuifanya benki hiyo kupata mafanikio makubwa na kushinda Tuzo za Kitaifa na Kimataifa, ikiwemo ya Mlipa Kodi Bora Mwaka 2024.
“Serikali ya Zanzibar inatambua na kuthamini mchango wenu katika makundi mbalimbali sio tu ya wajasiriamali, wafanyabiashara na wateja wenu kwa ujumla, bali pia Watoto Yatima na Wanaoishi Mazingira Magumu, moyo huo ndio siri wa mafanikio makubwa mnayoyapata siku hadi siku.
“Tunatamani kuona taasisi nyingi, wadau mbalimbali wakijitokleza kufuata nyazo za NMB katika kuwashika mkono watoto wenye uhitaji nchini ili kuwaendeleza katika maisha yao, jambo hili sio tu linaleta furaha ma ujira mwema, bali linatusukuma kukumbuka wajibu wetu wa kusaidiana,” alisema Spika Maulid katika hafla hiyo.
Alibainisha ya kwamba, mfululizo wa hafla za iftar kila mwaka katika mikoa mbalimbali nchini, ni ishara njema ya namna NMB inavyoweka mbele maslahi mapana ya jamii, yakiwemo makundi ya watu wenye uhitaji, huku akiitaka kudumisha utamaduni huo na kushirikiana na Serikali katika kuiletea jamii maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw. Juma Kimori, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki hiyo, Bi. Ruth Zaipuna, aliishuru SMZ kwa ushirikiano mkubwa inatoa kwa taasisi yake na kwamba ujio wa viongozi waandamizi na uwingi wa waalikwa, unaakisi imani na heshima kubwa waliyonayo kwa benki yake.
“Kukusanyika pamoja nyakati za mfungo wa Ramadhan, umekuwa ni utamaduni endelevu wa benki yetu, lengo likiwa sio tu kujumuika pamoja na wateja wetu, viongozi wa dini, Serikali na watoto wenye uhitaji, bali pia kustawisha mahusiano mema baina yetu na jamii na pia kudumisha ukaribu na hii ni faraja kubwa kwetu.
“Kufanya hivi, tunajaribu kuiishi kaulimbiu yetu isemayo: Karibu Yako, kwani mahusiano mazuri kati ya NMB na wateja wetu, sambamba na wadau mbalimbali, yamekuwa chachu ya mafanikio yetu na ndio maana tunautumia mwezi huu kukutana nao, huku tukikumbushana umuhimu wa kutenda yaliyo mema.
“NMB tunaona ipo haja ya kutumia mwezi huu kutafakari kwa pamoja mazuri yote ambayo Mungu ametujaalia, kuendelea kuwa watu wema, wenye kushiriki matendo yanayompendeza Mungu ndani ya mfungo wa Ramadhani na hata baada ya mfungo,” alibainisha Bw. Kimori mbele ya waalikwa zaidi ya 600 waliohudhuria Iftar hiyo.
Aliongeza ya kwamba anaamini kusanyiko hilo lililojumuisha Watoto Yatima wanaolelewa na Vituo vya Kidundo na Muftuh, ni fursa inayoenda kuacha alama mioyoni mwa watoto hao, kwani limewapa fursa nzuri na muhimu ya kujifunza na kuhamasika kutenda mema na kuwa wakarimu kwa jamii inayowazunguka.
“Kama tulivyofanya Dar es Salaam tulikofuturisha watoto kutoka vituo viwili, pamoja na iftari hii leo, NMB tunaahidi mbele yako Mheshimiwa Spika ya kwamba, tutaendelea kusaidia vituo hivi na watoto wake wote katika kipindi chote cha Ramadhan na hapa leo tunao msaada wa vyakula tutavyokukabidhi, nawe uvikabidhi kwao,” aliongeza Bw. Kimori.
Kwa nyakati tofauti, walezi wa Kidundo Orphanage Center na Muftuh Foundation Center, Khalid Idd na Idrisa Juma Kombo, waliishukuru NMB sio tu kwa kuwaalika katika hafla hiyo, bali kujitoa kusaidia mahitaji na huduma za watoto wa vituo vyao katika kipindi chote cha Ramadhani, huku wakizitaka taasisi zingine kufuata nyayo za benki hiyo.
“Kwetu sisi kama Kidundo, hii sio mara ya kwanza kwa NMB kutushika mkono, ndio maana tunapowashukuru na kuwapongeza kwa kutujali na kusaidia utatuzi wa changamoto zetu, tunaona ipo haja ya taasisi zingine kufuata nyayo hizo katika kuwaangalia watoto hawa kwa jicho la huruma,” alisema Khalid Idd Haji wa Kidundo chenye watoto 30.
Naye Kombo wa Muftuh Foundation, alisema: “Tunaishukuru NMB kwa kutufuturisha, lakini pia kwa sadaka kubwa iliyotoa na iliyoahidi kutupatia katika mwezi mzima wa Ramadhani. Changamoto kwa watoto wetu (76) tulionao ni nyingi ndio maana tunapopata msaada kama huu tunafurahi na kuomba taasisi zingine nazo zifuate nyayo za kutusaidia malezi.”
Mwisho
Comments