SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Sais Samia Suluhu Hassan, imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 426.3 kupitia Wakala wa Maji Vijijini, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma na Mamlaka ya Maji ya Mgango- Kiabakari.
Miradi mikubwa ya maji iliyotekelezwa mkoani humo ni pamoja na mradi wa Mgango -Kiabakari- Butiama wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5 ambao umekamilika, Rorya-Tarime wenye thamani ya shilingi bilioni 134.4 ambao umeanza kutekelezwa na mradi wa Mji wa Mugumu wenye thamani ya dola za marekani milioni 8.75 ambao umeanza kutekelezwa.
Hato yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma Julai 18, 2025, kuhusu mafanikio ya mkoa huo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umeongezeka kutoka asilimia 54 mwaka 2021 hadi asilimia 81 Juni, 2025. Upatikanaji wa maji safi na salama katika miji unaridhisha na hadi kufikia Juni, 2025 upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Musoma ni asilimia 98, Mji wa Mugumu asilimia 67, Mji wa Tarime asilimia 77 na Mji wa Bunda ni asilimia 86," amesema .Kanali Mtambi.
Aidha, serikali inatekeleza miradi ya majitaka miwili ambapo imechimba mabwawa ya kusafishia maji taka katika Manispaa ya Musoma wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 33 na mradi wa majitaka wa Butakale katika Mji wa Bunda wenye thamani ya shilingi bilioni 1.728 ambao unaendelea kutekelezwa.
Comments