SERIKALI YAIPONGEZA NMB KUCHANGIA MIL. 30 TAIFA STARS CHAN2024

SERIKALI imeishukuru na kuipongeza Benki ya NMB, kwa mchango wa Sh. Mil. 30 iliyoutoa kuhamasisha mashabiki na wachezaji wa Taifa Stars kuelekea mechi ya robo fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Nyota wa Ndani (CHAN 2024), dhidi ya Morocco, itakayopigwa Ijumaa Agosti 22, jijini Dar es Salaam.
 
Sambamba na pongezi hizo, Serikali imewataka wadau, makampuni, mashirika na taasisi binafsi na za umma, kufuata nyayo za NMB, ambayo ameitaja kama iliyoonesha njia kwa vitendo kusapoti jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anaendelea kuipa Taifa Stars zawadi ya Sh. Mil. 10 ya Goli la Mama kwa kila ushindi.
 ‎
‎Shukrani na pongezi hizo kwa NMB, pamoja na wito kwa wadau, vimetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, wakati akipokea hundi ya mfano ya Sh. Mil. 30 zilizotolewa na NMB, mbele ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha.
 ‎
‎Kati ya fedha hizo za NMB, Sh. Mil. 20 zitatumika kununulia tiketi za mashabiki 10,000 wa kuingia uwanjani kuwashangilia wachezaji, huku Sh. Mil. 10 zikiwa ni motisha kwa wachezaji wa kikosi hicho kinachocheza robo fainali ya kwanza katika michuano ya Mataifa ya Afrika, kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na waandishi wa Habari, Msigwa aliishukuru NMB kwa mchango huo wa mapema kuelekea robo fainali hiyo ya Ijumaa na kwamba ilichofanya ni kumuunga mkono Rais Samia, ambaye ni mhamasishaji namba moja wa Taifa Stars na michezo kwa ujumla.
 
“Serikali inawashukuru sana NMB, fikisheni salamu za Serikali kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, inakwenda kumuorodhesha kama mmoja wa wanamichezo mahiri na wa kupigiwa mfano kwa nchi yetu.
 
“NMB ni ndugu zetu na tunasema kwamba tunathamini mno mchango wao huu mkubwa, tunaahidi kuendeleza mashirikiano mema na ninyi na bahati mzuri mmesema hapa kuwa ushirikiano huu utaendelea. NMB ni benki yetu na hili walilokuja kusapoti ni jambo lao na sisi Watanzania tunapaswa kuisapoti NMB,” alisema Msigwa.
 
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa: “Pamoja na kuwashukuru NMB kwa kutuchangia Sh. Mil. 30, tunawaomba wadau wengine wote kuunga mkono juhudi hizi za kufanikisha timu kufanya vema na kutwaa ubingwa, ambao ukija nyumbani utakuwa wa Watanzania wote, basi hatuna budi kujitokeza kuichangia timu hii.
 
“Wakati wa kuonesha hilo ni sasa na sio wakati mwingine, fursa hii imekuja kwa mara ya kwanza, kwani Tanzania haijawahi kupata mafanikio makubwa kama haya. Kwahiyo kama ambavyo NMB imeonesha njia, wadau wengine wafuate nyayo,” alisisitiza Msigwa na kuongeza kuwa ahadi na michango ya majirani zetu, iwe somo kwa Watanzania.
 
Awali, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard, alisema benki yake imevutiwa na mafanikio ya Taifa Stars kiasi cha kuwiwa kuwaunga mkono kwa kuwachangia Sh. Mil. 30 kuonesha kujali na kuthamini kujitoa kwao na kuliheshimisha taifa kwa rekodi ya kipekee.
 
“Tuko hapa kuonesha uungaji mkono wetu kwa Taifa Stars, mchango ambao umegawanyika katika sehemu mbili; kwanza tunakabidhi Sh. Mil. 20 za kununulia tiketi 10,000 za mashabiki wa kushangilia timu kwenye robo fainali dhidi ya Morocco, lakini pili tunatoa Sh. Mil. 10 kama motisha kwa nyota wetu.
 
“NMB tunaamini kuwa mchango huu utasaidia kuwapa ari ya upambanaji wachezaji wetu ili kufanya vizuri na kuvuka hatua moja baada ya nyingine, tukianza na robo fainali hiyo. Kama kaulimbiu yetu kuelea CHAN inavyosema; ‘Litakuja Nyumbani’ basi vijana wahamaiske kulileta,” alisema Donatus.
 
Aliongeza ya kwamba, benki yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili kuhakikisha Taifa Stars inaendelea kufanya vizuri na mchezo wa soka unapiga hatua.
 

 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

WALIOKUWA WABUNGE WALIOPITIWA NA MKASI WA WAJUMBE

SPIKA MSTAAFU NDUGAI AFARIKI DUNIA

USAJILI ULIVYO HADI SASA....

MWENYE MASIKIO NA ASIKIE....

RAIS SAMIA AMUONDOLEA POLEPOLE HADHI YA UBALOZI

RAIS SAMIA AYATAKA MASHINDANO YA MISS WORLD 2027

RAIS WA BURKINA FASO ATANGAZA DIRA YA KUUNDA MUUNGANO WA MATAIFA YA AFRIKA (UNITED STATES OF AFRICA).