MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, sasa itafunguka kibiashara kutokana na uwepo wa kituo cha Treni ya SGR na ujenzi wa Bandari kavu.
Ameyasema hayo aliposimama kwa muda kuwasalimia wananchi wa Bahi Mjini, mkoani Dodoma akielekea Mkoani Singida kuendelea na kampeni zake kwa kwanzia Wilaya ya Manyoni, Ikungi na Singida Mjini.
Aidha, Dkt. Samia pamoja na mambo mengine ameahidi kwamba endapo wananchi watampatia ridhaa ya kuongoza nchi kwa kupigiwa kura Oktoba 29, 2025, Serikali itaendelea kuifanyia marekebisho makubwa Skimu kubwa ya umwgiliaji ya zao la mpunga iliyopo wilayani humo Ili wakulima waweze kulima zao hilo mara mbili kwa mwaka.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, ametumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho.
Baada ya uzinduzi wa kampeni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe Jijini Dar es Salaam, leo Mgombea huyo anaingia kwa kishindo mkoa wa saba wa Singida baada ya kufanikisha kwa kiwango kikubwa kampeni katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
Comments