MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais, DKT. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuanza kwa majaribio utoaji wa huduma mpya ya Bima ya Afya kwa wote ndani ya siku 100 baada kupata ridhaa ya wananchi kuongoza tena nchi.
Amesema kuwa endapo wananchi watamchagua katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, ndani ya siku hizo 100 Serikali itaanza majaribio katika baadhi ya maeneo na ikifanikiwa itafanyika kwa nchi nzima.
Aidha, DKT. Samia ameongeza kuwa katika Wilaya hiyo, watajenga Chuo Cha Ufundi Stadi VETA, kuendeleza ujenzi wa barabara inayounganisha Mkoa wa Singida na Mbeya pamoja na kujenga kituo Cha TBC ili kuongeza usikivu.
Ameyasema hayo aliposimama kuwasalimia wananchi katika Mji wa Manyoni, akielekea Ikungi na hatimaye kwenye mkutano mkubwa wa kampeni Singida mjini. Kabla ya Manyoni amewasalimia pia wananchi wa Bahi mkoani Dodoma.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, atatumia fursa hiyo kuwanadi wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho. Jana amefanya kampeni katika Mji wa Mbalizi na Mbeya Mjini.
Baada ya uzinduzi wa kampeni kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe Jijini Dar es Salaam, leo Mgombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia kwa kishindo mkoa wa saba wa Singida baada ya kufanikisha kwa kiwango kikubwa kampeni katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
Comments