Kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Rais Dkt Samia Suluhu Hassan leo zinafanyika Buza Tanesco wilayani Temeke, Dar es salaam baada ya kufanikisha katika Wilaya za Ubungo, Kinondoni na Ilala.
Kampeni za leo zitashirikisha Wilaya mbili za Temeke na Kigamboni zenye majimbo manne ya uchaguzi ya Temeke, Chamazi, Mbagala na Kigamboni.
Baada ya kuhitimisha kampeni leo kwa Mkoa wa Dar es salaam, Dkt. Samia atavuka Bahari ya Hindi kwenda kwenda kuomba kura Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar na hatimaye kufunga Kampeni Rocky City Mwanza.
Akiwa katika mikutano hiyo, Dkt. Samia hujinadi kwa kuelezea mafanikio makubwa ya miradi ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na mitano ya Tanzania Visiwani, pia hutoa ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa miaka mingine mitano endapo atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.
Aidha, Dkt. Samia amekuwa akisisitiza kudumisha Muungano na kuendelea kulinda amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Pia amewatoa wananchi wasiwasi kwamba hakutokuwa na vurugu kwani vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko imara, hivyo siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi tena bila hofu kwenda kupiga kura na kurejea salama majumbani.
Pamoja na kuelezea kwa undani Ilani ya uchaguzi ya chama hicho, Dkt. Samia ambaye mgombea wake mwenza ni Dkt. Emmauel Nchimbi, hutumia fursa hiyo kujinadi yeye, wagombea ubunge na madiwani wa chama hicho.
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA-0754264203
Comments