BODABODA ALIPWA PIKIPIKI BAADA KUSAFIRI KWA BODA KWA SAA 10 MBEYA HADI DAR

Kijana dereva wa bodaboda anayefahamika kwa jina la Brown Anthony ameibua gumzo kubwa miongoni mwa wananchi baada ya kufanikiwa kusafiri kutoka jijini Mbeya hadi Dar es Salaam kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer 150 HD yenye namba ya usajili MC 473 FKT, ndani ya saa 10, safari iliyoanzia kwenye ubishani wa kawaida na kuhitimishwa kwa ushindi wa kihistoria.


Ubishani huo ulianza tarehe 14 Januari 2026 kati ya Brown Anthony na bodaboda mwenzake Alex Ndile, ambapo walitofautiana kuhusu uwezekano wa kufika Dar es Salaam kwa pikipiki ndani ya muda wa masaa 13. Baada ya majadiliano makali, walikubaliana kuyaweka madai yao katika makubaliano rasmi ya kisheria.

Makubaliano hayo yaliwekwa mbele ya mwanasheria Ambakisye Kibona, ambapo kila mmoja alikuwa na pikipiki yake binafsi, na pande zote zilikubaliana kuwa atakayeshindwa atalazimika kumpa mshindi pikipiki yake kama dau la makubaliano hayo.

Baada ya makubaliano kukamilika, Brown Anthony alianza safari yake rasmi tarehe 15 Januari saa 11:00 asubuhi, akitokea Mbalizi jijini Mbeya, akitumia pikipiki yake kama ilivyokubaliwa katika makubaliano hayo ya kisheria.

Katika safari hiyo ndefu na yenye changamoto, Brown Anthony alifanya mapumziko mara tatu kwa ajili ya ukaguzi na matengenezo madogo ya pikipiki, hatua iliyomwezesha kuendelea na safari bila matatizo ya kiufundi.

Hatimaye, alifanikiwa kuwasili jijini Dar es Salaam saa 9:35 alasiri siku hiyo hiyo, akitumia muda uliokuwa chini ya masharti ya makubaliano, na hivyo kuthibitisha ushindi wake dhidi ya mpinzani wake Alex Ndile.

Baada ya kukamilisha safari hiyo, Brown Anthony alianza safari ya kurejea Mbeya alfajiri ya saa 11 kutoka Dar es Salaam, na kufanikiwa kuingia Mbalizi jijini Mbeya jioni ya Ijumaa, Januari 16, 2026, ambapo alipokelewa kwa shangwe. Kufuatia ushindi huo, alikabidhiwa pikipiki ya ushindi, iliyokuwa mali ya Alex Ndile yenye namba ya usajili MC 695 EFE.



 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

MAPACHA WATATU FAMILIA YA MWAIKENDA WAPATA KIPAIMARA

MVUA KUBWA KUNYESHA MIKOA 20

AINA 4 ZA WANAWAKE WASIOWEZA KUDUMISHA NDOA.

MIKOA 10 YENYE KIPATO KIKUBWA ZAIDI KWA MTU MMOJA MMOJA

IJUE HISTORIA YA MCHEZAJI MZUNGU WA TANZANIA