Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imepiga hatua kubwa katika kusambaza huduma ya maji vijijini, ambapo hadi sasa huduma hiyo imefika katika vijiji 10,758 kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini.
Aweso ametoa kauli hiyo wakati akizungumzia mafanikio ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi chake cha pili, akieleza kuwa juhudi kubwa zimeendelea kufanywa na Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.
Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo, vijiji 1,575 bado havijafikiwa na huduma ya maji, lakini Serikali inaendelea na mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kufikisha huduma hiyo katika maeneo yaliyosalia.
"Nchi yetu ya Tanzania ina Vijiji 12,333. Mpaka sasa Wizara ya Maji imeshafika Vijiji 10,758. Vijiji vilivyobakia ni 1,575." - Jumaa Aweso, Waziri wa Maji
Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha vijiji vyote vilivyobakia vinafikiwa na huduma ya maji kwa awamu, sambamba na kuimarisha miundombinu ya maji ili huduma iwe endelevu na yenye ubora.
Aidha, ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi, hususan walioko vijijini.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Baadhi ya waandishi wa habari pamoja na viongozi wa serikali.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akifafanua jambo alipokuwa akihitimisha mkutano huo.
Aweso akisindikizwa baada mkutano huo kumalizika.
Comments