WANANCHI zaidi milioni 8.5 hususan wanaoishi Vijijini na mipakani wanatarajiwa kuondolewa changamoto ya mtandao, baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuzindua minara 758 na maunganisho ya mkongo wa mawasiliano katika wilaya 85 pamoja na kukabidhi mkongo wa mawasiliano serikalini iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo leo leo Aprili 10, 2026 jijini Dodoma,Rais Samia amesema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” amesema.
Aidha Rais Samia amezitaka halmashauri zote nchini kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya miradi ya mawasiliano ili kuharakisha utekelezaji wake, akibainisha kuwa ucheleweshaji huongeza gharama na kuchelewesha huduma kwa wananchi.
Rais Samia amesisitiza kuwa mawasiliano sasa ni nguzo muhimu ya uchumi wa kisasa, uwekezaji na utoaji wa huduma za kijamii, hivyo yanahitaji kupewa kipaumbele katika ngazi zote.
Hata hivyo Rais Samia pia ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na Mkongo wa Taifa yanaunganishwa kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili kuendana na mahitaji ya sasa ya teknolojia.
Ameitaka sekta husika kuhakikisha huduma zinazotolewa kupitia miundombinu hiyo zinazingatia maadili, mila na utamaduni wa Mtanzania, ili kulinda utambulisho wa taifa katika enzi hii ya utandawazi.
Rais Samia ameongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya Tehama ni muhimu kwa mustakabali wa uchumi wa taifa,hasa katika kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kidigitali katika sekta mbalimbali.
“Tutatenga fedha maalum zitakazowezesha Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuzipatia mitaji kampuni changa za vijana (startups) ili ziweze kukua zaidi”amesema Rais Samia
Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Kairuki, amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya mawasiliano na TEHAMA ili kuhakikisha inakuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Waziri Kairuki amemshukuru Rais Samia kwa uongozi wake thabiti na mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya mawasiliano, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya maelekezo na usimamizi wake wa karibu.
“Sekta ya mawasiliano ni mhimili muhimu unaowezesha sekta nyingine kama afya, elimu, kilimo na biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kumekuwa na ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma za mawasiliano, intaneti na huduma za kifedha kidijitali, hatua inayoonesha kukua kwa kasi kwa uchumi wa kidijitali nchini.”amesema Waziri Kairuki
Aidha, amesisitiza kuwa Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali na Mkakati wa Taifa wa Mtandao wa Kasi, huku akiahidi kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mipya ikiwemo ujenzi wa minara zaidi na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa wananchi wote kwa gharama nafuu na ubora wa hali ya juu ili kuchochea ajira, ubunifu na ushindani wa kimataifa.
Awali Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na umegharimu shilingi bilioni 126,ambapo bilioni 55 ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali na bilioni 71 ni fedha za ndani kupitia UCSAF.
“Mradiu huo umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali kupitia UCSAF na kampuni za simu nchini,ambapo ruzuku ya serikali imetumika kuchochea uwekekezaji katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za Mawasiliano”amesema Mhandisi Mwasalyanda

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla akisaini Hati ya Makabidhiano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yas Tanzania Bw. Pierre Canton-Bacara (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Bw. Charles Kamoto wa kwanza (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Bw. Andrew Lupembe katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Kairuki pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Wizara hiyo, Mbunge wa Mtama Mhe. Nape Nnauye kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2026. Rais Dkt. Samia alipewa zawadi hiyo kutokana na kutambua mchango wake kwenye Sekta hiyo ya Mawasiliano.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya wadau wa Sekta ya Mawasiliano katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kabla ya Uzinduzi wa minara 758, maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano katika Wilaya 85 na kukabidhi Mkongo wa Mawasiliano Serikalini, tarehe 10 Aprili, 2026.






Comments