Watanzania wameshauriwa kujivunia nchi yao kuongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kutokana na kusimamia utawala bora katika uendeshaji wa serikali.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Mary Chatanda, Oktoba 7, 2026, katika Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kumalizika kikao cha baraza la vyama vya siasa.
Ameeleza kuwa, Rais Dk. Samia ni muumini wa ushirikishwaji wa makundi muhimu ya jamii ili kuhakikisha maendeleo jumuishi yanapatikana.
"Rais wetu ameendelea kukaa meza moja na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini ili kuimarisha umoja na mshikamano kwa mustakabali mwema wa ujenzi wa taifa," amesema Chatanda.
Amesisitiza kuwa, kiongozi aina ya Dk. Samia ni wa kumlinda kwa wivu mkubwa na zaidi ya yote kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema ili awatumikie vyema wananchi.
"Kama nchi tuna kila sababu ya kuona fahari kuwa na Rais aina ya Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye uongozi na utawala bora vimekuwa msingi wa uongozi wake," amesema.
Sambamba na hilo, Chatanda amesisitiza kuwa, uongozi wa Dk. Samia unatambulika kimataifa, ndiyo maana Rais wa Wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Cynthia Lopez, amemtaja Rais Dk. Samia kuwa mfano wa kiongozi bora mwanamke.
Ni kwamba, Oktoba 5, 2026, akihutubia Mkutano wa 153 wa IPU jijini Arusha, Lopez alimpongeza Rais Dk. Samia kwa uongozi bora huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika vyombo vya maamuzi.
"Tunapokuwa na wanawake wengi zaidi katika mabunge, tunakuwa na nguvu na ushawishi zaidi. Tuna wanawake wanaongoza kamati, tuna maspika wanawake na tuna viongozi wanawake, kama Rais wa Tanzania, Rais Samia," amesema Lopez.

Comments