TAASISI ZA MICHEZO ZATAKIWA KUTUMIA MILIKI UBUNIFU KUDHIBITI UHARAMIA

 

 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA,  Godfrey Nyaisa warsha maalumu kwa wadau wa michezo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi jijini Dar es Salaam .

NA MWANDISHI WETU 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umezitaka Taasisi, Mashirikisho na Vyama mbalimbali vya michezo nchini kutumia Miliki Ubunifu kuhakikisha inadhibiti uharamia unaofanyika katika sekta michezo nchini ili kukuza na kuimarisha sekta hiyo.


Wito huo umetolewa leo  Oktoba 6, 2026 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA,  Godfrey Nyaisa wakati akifungua warsha maalumu kwa wadau wa michezo nchini iliyofanyika katika ukumbi wa King Jada Jijini Dar es Salaam ambapo aliwataka pia wadau wa michezo kuongeza uelewa kuhusu namna ya kulinda na kutumia ubunifu kukuza michezo.



“Kimsingi, sioni sababu ya kushindwa kudhibiti jezi feki, skafu feki, beji feki na bendera feki za vilabu vya michezo zinazouzwa pembezoni mwa viwanja vya mpira wakati wa mechi au hata kwenye masoko makubwa kama kariakoo Dar es Salaam. Suala hili lipo ndani ya uwezo wetu kabisa, suluhisho pekee la kudhibiti uharamia huu ni kupitia Miliki Ubunifu na vyombo vy Serikali na wahusika wenyewe” alisema Nyaisa



Awali akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyoandaliwa na BRELA kwa wadau wa michezo nchini, Bw. Nyaisa alisema matumizi ya picha za wanamichezo ambao wana mikataba na vilabu au taasisi husika kwa sasa limekuwa tatizo, na kwamba huwezi kutumia picha za wanamichezo kibiashara bila kuwa na makubaliano maalumu na vilabu au taasisi ambazo wanamichezo hao wanazitumikia. 



Kwa upande wake Ofisa Sheria kutoka Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Thadeus Almas akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza hilo Bi. Neema Msitha alisema warsha hiyo ni muhimu kwa sekta ya michezo nchini na kwamba Baraza litaendelea kushirikiana na BRELA kuhakikisha elimu wanayoipata wadau hao inakwenda kusaidia kukuza na kuendeleza sekta ya michezo na kuinua hadhi ya vilabu, mashirikisho na vyama mbalimbali vya michezo.



“Kwa sasa kuna kampuni nyingi za michezo ya kubashiri, lakini Je, sekta ya michezo inanufaika vipi? vilabu vyetu vinapata faida gani, huu ni wakati sasa wa Mashirikisho yetu kuhakikisha tunafaidika na kampuni hizo, sisi kama Baraza, tunaendelea kushirikiana kwa karibu na BRELA kuhakikisha elimu hii inawafikia mashirikisho na vyama vya michezo nchini ili kuhakikisha wachezaji wananufaika na bunifu zao, mfano hizi kampuni za michezo ya kubashiri zinapaswa kuingia makubaliano na shirikisho letu kuhakikisha vilabu vyetu vipata faida na sekta nzima inanufaika.” alisisitiza Bw. Almas



BRELA imeandaa warsha hiyo ya siku moja na kuwakutanisha wadau wa michezo nchini ikiwemo taasisi mbalimbali za michezo ikiwemo Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania COSOTA kwa lengo la kuwaongeza uelewa kuhusu masuala ya Miliki Ubunifu na kuhakikisha bunifu zinaozalishwa katika sekta ya michezo zinalindwa na kutumika kama sehemu ya kuchochea maendeleo ya Taifa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

𝐌𝐉𝐔𝐄 𝐊𝐀𝐂𝐇𝐄𝐑𝐎 𝐌𝐙𝐄𝐍𝐀

KATIKA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA.

YANGA YAMPOTEZA MAMA FATMA KARUME MWANA YANGA KINDAKI NDAKI

MVUA ZA EL NINO ZINASABABISHWA NA NINI?.