NA MWANDISHI WETU
Katika kuimarisha mazingira salama ya kujifunza na kufundisha kwa wanafunzi wa shule za sekondari, washiriki 420 kutoka mikoa saba nchini wameanza mafunzo ya Mpango wa Shule Salama yanayolenga kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, kuboresha mazingira ya shule na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora pamoja na stadi za maisha.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Maria Lyimo aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa Mkoa wa Iringa amewataka washiriki kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa Mpango wa Shule Salama baada ya mafunzo hayo kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na jamii, ili kuwa chachu ya kuboresha mazingira ya mtoto shuleni.
Aidha Mratibu wa Mpango wa Shule Salama kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Hilda Lazaro amesisitiza umuhimu wa waratibu kusimamia utekelezaji wa mpango huo kwa kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira rafiki na salama, ikiwemo kuboresha miundombinu na kuweka mifumo madhubuti ya kuzuia na kushughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Shule, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa jamii, ambao wanatarajiwa kutumia maarifa watakayoyapata kuimarisha utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao.




Comments