KIKWETE NA UN, AU KUONGOZA MCHAKATO WA AMANI SUDANI KUSINI

Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, ameteuliwa kuongoza  Timu ya Pamoja ya Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika (IGAD) itakayoshughulikia mchakato wa amani nchini Sudan Kusini.

Timu hiyo imeundwa kwa mapendekezo ya Kamati ya Marais wa Nchi Tano ya Umoja wa Afrika inayoshughulikia amani ya Sudani Kusini (C5) ambao ni Marais wa Afrika Kusini (Mwenyekiti) Nigeria, Rwanda, Algeria na Chad, katika Mkutano wao uliofanyika tarehe 29 Septemba, 2026. 

Kwa sasa Kikwete tayari ni Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu na pia amewahi kufanya ziara nchini Sudan Kusini kama Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika kwenye mazungumzo ya kutafuta amani nchini Sudan. 

Timu hiyo inaundwa na Rais Mstaafu Dkt. Kikwete ambaye anauwakilisha Umoja wa Afrika, Anita Kiki Gbeho ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) pamoja na Balozi Moussa Djama Ali, ambaye ni Mjumbe Maalum wa IGAD nchini Sudan Kusini. 

Hafla hiyo fupi ya kuzindua Timu hiyo ilihudhuriwa pia na Cecilia Adut Manyok, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudani Kusini, pamoja na Balozi Meja Jenerali (Mstaafu) George Aggrey Owinow, Mwenyekiti wa Muda wa Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini ya masuala ya Amani nchini Sudani Kusini (RJMEC). Viongozi hao watasaidiwa na kamati za wataalamu kutoka katika Mashirika hayo ya Kimataifa.
Akizindua timu hiyo jijini Addis Ababa, Ethiopia leo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ameeleza matumaini yake kuwa ushirikiano huo baina ya mashirika hayo ya kimataifa utaongeza chachu ya kukamilisha mapema mchakato wa kupata amani ya kudumu nchini Sudani Kusini.


 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

TUCTA WAPATA RAIS MPYA

TIMU YA NGORONGORO KAMA DOUMBIA

KAMISHNA DKT.BADRU ATUA KAMBI YA TIMU YA NGORONGORO KAMA SELEMANI MWALIMU