MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA


NA MWANDISHI WETU


Serikali imesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI, ikiwemo kupunguza maambukizi mapya kutoka watu 98,754 mwaka 2010 hadi 33,511 mwaka 2025, huku vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vikishuka kutoka watu 55,833 hadi 25,995 katika kipindi hicho.


Hatua hiyo imetokana na juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali pamoja na wadau wa afya katika kuimarisha huduma za kinga, upimaji na matibabu, ikiwemo upatikanaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) zinazotolewa bila malipo kwa wananchi.


Akizungumza leo Novemba 19, 2026 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema mafanikio hayo yanaonesha mwitikio wa Taifa katika kudhibiti maambukizi ya VVU na kupunguza athari za ugonjwa huo.


Amesema maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu yataanza Novemba 24 katika kanda saba za Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na kuhitimishwa Desemba Mosi, 2026 katika ukumbi wa Jakaya Convention Centre jijini Dodoma, yakiongozwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye atakuwa mgeni rasmi.



Amesema takwimu za kidemografia kupitia mfumo wa DHIS-2 zinaonesha kuwa hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wamepima na kutambua hali zao, huku asilimia 99.5 ya waliotambua hali zao wakipata huduma za dawa za ARV na asilimia 98.2 ya wanaotumia dawa hizo wakiwa wamefubaza virusi mwilini.


Profesa Kabudi amesema pia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 9.1 mwaka 2010 hadi asilimia 6.2 mwaka 2025, hatua inayoonesha mafanikio katika huduma za afya ya uzazi na udhibiti wa maambukizi.


Hata hivyo, amebainisha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 bado ni kundi linalohitaji kupewa kipaumbele katika mapambano hayo, akieleza kuwa wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya ya VVU, huku asilimia 77.7 ya maambukizi hayo yakiwa miongoni mwa vijana wa kike.


Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa vijana kuwajibika katika kujikinga na VVU, kupima ili kujua hali zao na kushiriki kutoa elimu sahihi kwa jamii, huku akisisitiza umuhimu wa kuondoa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU.



Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yataambatana na kumbukumbu ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa TACAIDS mwaka 2001, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji”, inayohimiza upatikanaji wa huduma, rasilimali na utashi wa kisiasa katika kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.


Aidha, Profesa Kabudi amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji wa rasilimali za ndani, kushirikisha sekta binafsi na kuendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kinga, upimaji na matibabu zinaendelea kupatikana bila kuathiriwa na mabadiliko ya ufadhili wa kimataifa.


Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ni jukumu la kila Mtanzania, akiwataka wananchi, taasisi za Serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini na vyombo vya habari kushirikiana katika kutoa elimu na kujenga jamii isiyokuwa na unyanyapaa.




Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

UJUE UKWELI KUHUSU JIJI LA MBEYA (GREEN CITY)

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

TIMU YA NGORONGORO KAMA DOUMBIA

KAMISHNA DKT.BADRU ATUA KAMBI YA TIMU YA NGORONGORO KAMA SELEMANI MWALIMU