Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 25 ya NHIF kupitia NHIF Marathon 2026 zilizoshirikisha takribani watu 10,000 jijini Dodoma, Mhe. Mchengerwa ameutambua mchango wa Mfuko katika kulinda afya za Watanzania, huku akiipongeza Bodi, Menejimenti na watumishi kwa kuendelea kuimarisha huduma na kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi.
Amesema dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha inaendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo takribani Shilingi bilioni 98 zimetolewa kwa ajili ya kugharamia huduma za afya kwa wananchi wasio na uwezo.
Aidha, amesema Serikali imepanua wigo wa upatikanaji wa bima kupitia kifurushi cha Shilingi 150,000 kwa kaya, kinacholenga makundi mbalimbali ya wananchi na kutoa fursa ya kupata huduma 372 za afya, kwa mujibu wa masharti ya kifurushi hicho.
Mchengerwa amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yanachangia zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya jumla ya NHIF, huku akiwataka viongozi wa mikoa na wilaya kuhamasisha jamii kuzingatia afya.
Amesisitiza kuwa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kila mdau ana wajibu wa kulinda afya za wananchi, akieleza kuwa kuimarisha bima ya afya, huduma za matibabu na kinga dhidi ya magonjwa ni msingi wa ustawi wa taifa.




Comments