NA MWANDISHI WETU
MRADI wa Kusaidia Utekelezaji wa Mitaala kwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (CISTI), unaotekelezwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), umenufaisha zaidi ya wanafunzi 2,000 wa Chuo cha Kilimo Tumbi kilichopo mkoani Tabora.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo hicho, Barnaba Makavu, wakati akizungumzia mradi huo ambao umekuwa na manufaa kwa wakufunzi, wanafunzi na wakulima.
Makavu alisema pia shirika hilo limewezesha uaandaji wa mitaala, mada maalum kama jinsia, upatikanaji wa vifaa ambavyo vinawawezesha walimu kufundisha kwa njia ya mtandao, kufanya mikutano na usahili kwa wanafunzi.
Mkuu huyo alisema shirika hilo limewajengea miundombinu ya green house ambayo wanafunzi na watumishi wanajifunza.
“Tangu CISTI ianze zaidi ya wanafunzi 2,000 wamepata mafunzo ambayo yanawawezesha kwenda kusadia wakulima vijijin, ambapo kila mwaka wahitimu wanafika 300,” alisema.
Alisema chuo kimekuwa kikiendelea kutoa elimu kwa wakufunzi na wanafunzi, ili waweze kuendana na dunia ya leo.
Mkuu huyo alisema maboresho ya mitaala ya kilimo ni muhimu kutokana na kuhusisha sekta ya kilimo na mifugo, ambazo zina mchango kwenye uchumi.
Makavu alisema kupitia Mradi wa CISTI wanafunzi wa Tumbi wameweza kuwafikia wakulima 4,000 gadi 5,000 jambo ambalo linawapa matumaini makubwa.
Ofisa Kilimo Chuo cha Kilimo Tumbi, Jeremia Obed alisema elimu ya SAT kwa wanafunzi imechochea mabadiliko mkubwa chuoni hapo.
Obed alisema SAT imekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya kilimo, hivyo ni wajibu wa kila mdau kushiriki mkutano huo.
Alisema kupitia program hizo wanafunzi wanasoma kilimo chuoni hao wataenda kusaidia wakulima anmbao wamekuwa wakitumia mbinu za zamani.
“Mradi wa CISTI umekuja wakati muafaka na umeweza kuleta mabadiliko changa, hasa katika eneo la mitaala, jambo ambalo tunaona linaenda kuleta mapinduzi ya kilimo,” alisema.
Meneja Mradi wa CISTI, Kashindye Salum alisema mradi huo ni mojawapo ya mipango muhimu ya SAT inayotekelezwa kwa kushirikiana na Idara ya Mafunzo na Utafiti (DTR) ya Wizara ya Kilimo.
“Tangu kuanza kwa mradi, SAT imekuwa ikishirikiana na DTR kuimarisha utoaji wa mafunzo yanayozingatia umahiri katika Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (ATIs), ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya soko la ajira na vipaumbele vya sekta ya kilimo,” alisema.
Meneja huyo alisema Mradi wa CISTI unaofadhili na Shirika la Maendeleo la Liechtenstein (LED), una lengo la kusaidia taasisi za mafunzo ya kilimo za umma na binafsi kuzalisha wataalamu wenye umahiri wa kiufundi, wanaoweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira, kueneza matumizi ya kilimo ikolojia na kuimarisha maisha ya wakulima wadogo na wafugaji.
Kashindye alisema katika kipindi cha 2019–2025, mradi umefikia jumla ya watu 26,297 moja kwa moja. Walengwa hao ni pamoja na wakulima 6,647, wakiwemo wakulima mabingwa 174 wa kilimo hai; wakufunzi na watumishi wa menejimenti 1,530; wahudumu wa bustani 117; na wanafunzi 18,003.
Alisema kuanzia mwaka 2019 hadi Awamu ya Kwanza (2020–2022), mradi ulichangia katika uandaaji na upatikanaji wa machapisho manane ya marejeo ya kitaaluma, ambapo nakala 4,200 zilichapishwa na kusambazwa.
Aidha, bustani za maonesho 29 zilianzishwa ili kuwezesha mafunzo kwa vitendo na kuimarisha upatikanaji wa stadi za kilimo.
“Awamu hii iliwafikia watu 12,427 moja kwa moja, wakiwemo wakulima 3,856 kupitia siku za wazi kwa wakulima zilizofanyika katika vyuo vya mafunzo ya kilimo, wakufunzi na wakuu wa vyuo 915, wahudumu wa bustani 117 na wanafunzi 7,539.
Walengwa hawa walinufaika kupitia upatikanaji bora wa nyenzo za kufundishia, kuimarishwa kwa uwezo wa wakufunzi na kuboreshwa kwa mazingira ya mafunzo kwa vitendo,”.
Kashindye alisema awa ya pili ililenga kuendeleza na kupanua maboresho ya utekelezaji wa mitaala inayozingatia umahiri katika vyuo vya mafunzo ya kilimo.
Alisema kipaumbele kilikuwa kuimarisha uwezo wa wakufunzi, kuongeza upatikanaji wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuboresha miundombinu ya mafunzo kwa vitendo ili kuzalisha wataalamu wenye stadi zinazohitajika.
“Katika awamu hii, mradi ulifikia vyuo 30 vya mafunzo ya kilimo na kuwanufaisha watu 13,870 moja kwa moja. Walengwa hao walijumuisha wakufunzi 394, watumishi wa menejimenti 221, wakulima 2,791 wakiwemo wakulima mabingwa 174, pamoja na wanafunzi 10,464,” alisema.
Pia mradi umeweza kuimarisha nyenzo za kufundishia na kujifunzia, mradi uliwezesha uandaaji na uthibitishaji wa machapisho mengine manane ya marejeo ya kitaaluma, ambapo nakala 3,060 zilichapishwa na kusambazwa.
Aidha, uliwezesha uandaaji wa vitabu vitatu vya kiada na miongozo minne ya mafunzo kwa vitendo, ambapo jumla ya nakala 2,170 zilichapishwa na kusambazwa.
Vilevile, mradi uliandaa Mwongozo wa Kilimo Hai kwa Kiswahili na kusambaza nakala 3,000 ili kuimarisha upatikanaji wa maarifa na ujifunzaji kwa wakulima.
Alisema mafunzo kwa vitendo yaliimarishwa kupitia uanzishwaji wa Vitalu nyumba (screenhouses) na bustani za maonesho 33, pamoja na ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kufundishia, vikiwemo vifaa vya mfumo wa GPS na chati za rangi za udongo za Munsell.
Aidha, mradi ulikamilisha maboresho ya miundombinu katika Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima cha SAT (SAT FTC), yaliyohusisha ujenzi wa vyumba 30 vya malazi vyenye huduma zote muhimu, mgahawa wenye samani na vifaa kamili, pamoja na ukumbi wa mafunzo.
“Mradi uliandaa na kurasimisha machapisho 16 ya marejeo ya kitaaluma ambayo ni ya kilimo hai, jinsia katika kilimo, usimamizi wa mazingira, stadi za msingi za mawasiliano, kanuni za ushirika katika kilimo, hisabati ya msingi katika kilimo, ugani wa kilimo na masoko ya klimo,” alisema
Pia ujasiriamali, uhifadhi wa udongo na maji, malisho na ulishaji wa Wanyama, lishe ya binadamu, utunzaji wa kumbukumbu katika kilimo, hatari za kikazi na usimamizi wa hatari katika kilimo, usimamizi wa miradi ya kilimo na usindikaji na uhifadhi wa mazao ya chakula.
Aidha, mradi uliandaa vitabu vitatu vya kiada vinavyohusu Kilimo Hai, Usimamizi wa Mazingira na Jinsia katika Kilimo, pamoja na miongozo minne ya mafunzo kwa vitendo katika maeneo hayo na Usindikaji na Uhifadhi wa Mazao ya Chakula, ambapo nakala 9,430 za machapisho zilichapishwa na kusambazwa katika taasisi za mafunzo nchini.




Comments