NA MWANDISHI WETU
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC Insurance) limeshika nafasi ya kwanza katika kundi la kampuni za bima kwenye Tuzo za NBAA 2026, zinazotambua ubora katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha.
Mkurugenzi wa Fedha wa NIC Insurance, CPA (T) Abdulkarim Kisuguru, alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Mkeyenge, katika hafla iliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) katika Viwanja vya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kisuguru alisema ushindi huo unaakisi juhudi za NIC za kusimamia fedha kwa weledi na kuwasilisha taarifa zake kwa uwazi. Alisema taarifa zilizoandaliwa vizuri huwasaidia wateja na wadau kuelewa jinsi shirika linavyotumia rasilimali zake na kuwajibika katika matumizi yake.
Katika kuandaa taarifa hizo, NIC huzingatia Viwango vya Kimataifa vya Utoaji wa Taarifa za Fedha (International Financial Reporting Standards, IFRS 17). IFRS 17 inaelekeza jinsi kampuni za bima zinavyotambua, kupima na kuwasilisha taarifa kuhusu mikataba ya bima.
Ushindi huo umejengwa juu ya maboresho ambayo NIC imekuwa ikifanya katika usimamizi wa fedha na utoaji wa huduma. Aidha, Shirika liko katika mwaka wa nne wa usimamizi wa mfumo wa ubora (ISO 9001:2015). Taratibu za kazi zilizo wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali husaidia kufuatilia miamala, kutunza kumbukumbu na kuandaa taarifa za fedha. Maboresho hayo pia yanarahisisha upatikanaji wa huduma za bima kwa wateja.
Sambamba na kutambuliwa kwa NIC kama Superbrand Afrika Mashariki kwa miaka minne mfululizo kunaakisi sifa ambayo shirika limejenga kwa wateja.
Mafanikio hayo ni uthibitisho wa juhudi za Shirika katika kudumisha ubora unaoonekana katika maeneo matatu ya *SISI NDIYO BIMA* yaani usimamizi wa shughuli zake na utoaji wa huduma kwa wateja.
Hatua hizo zinaendana na utekelezaji wa Dira 2050. Uwazi katika taarifa za fedha na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali vinaimarisha utawala bora. Kwa upande wa nguzo ya Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani, matumizi ya teknolojia kurahisisha upatikanaji wa bima yanasaidia wananchi na biashara kujilinda dhidi ya hasara zinazoweza kuvuruga shughuli zao za kiuchumi.



Comments