SERIKALI KUANZISHA MFUKO MAALUMU KUENDELEZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 


NA MAGENDELA HAMISI

SERIKALI imepanga kuanzisha mfuko maalumu wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kupanua fursa za uwekezaji na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi hususani vijijini.


Hayo yamebainishwa leo Ikulu jijinj Dar es Salaam na Waziri wa Nishati , Dkt Juma Homera wakati akitoa tathimini ya mafanikio ya ziara iliyofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki,  amefafanua kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na wawekezaji wamekaribishwa kuja nchini.


Aidha amesema kwamba Mfuko wa Nishati Safi ambao utahusisha Halmashauri zote nchini kupitia vikundi vitawezeshwa kutengezeneza majiko banifu na mkaa mbadala utasaidia kulinda mazingira kupitia taknolojia hiyo.


" Mkakati huo unalenga kuwawezesha vijana na wajasiriamali wanaojihusisha na utengenezaji wa majiko banifu, mkaa mbadala na teknolojia nyingine za nishati safi kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao na kusambaza bidhaa hizo nchini," amesema


Ameongeza kuwa mfuko huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.


Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa mfuko maalumu kutasaidia kufikisha huduma na teknolojia hizo hadi maeneo ya vijijini ambako matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida bado yanasababisha changamoto za kiafya na uharibifu wa mazingira.


Amesema kupitia ziara hiyo, Tanzania imeendelea kupata fursa za ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa katika kuendeleza teknolojia za nishati safi, ikiwemo uwekezaji katika uzalishaji wa teknolojia hizo na kupanua matumizi yake katika taasisi za umma, shule na vituo mbalimbali nchini.


Aidha, amesema kuna mpango wa kushirikiana na taasisi za elimu na vyuo vya ufundi, ikiwemo Chuo cha Ufundi Arusha na taasisi za teknolojia kutoka India, kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu teknolojia za nishati safi ya kupikia.


Katika kuimarisha juhudi hizo, amesema Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonesha utayari wa kuimarisha ushirikiano na Tanzania ili kupanua matumizi ya teknolojia za nishati safi katika taasisi mbalimbali, hususan shule na vituo vya umma.


Ameeleza kuwa pia kuna fursa za ufadhili na ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ya nishati ya jua na mifumo mingine ya nishati safi, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa nishati kwa wananchi.


Amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali kuimarisha mahusiano na taasisi za kifedha na maendeleo duniani, ambazo zimeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa teknolojia, ujenzi wa miundombinu na upanuzi wa matumizi ya nishati safi.


Pia amekumbusha kwamba matumizin ya umeme nchini yameongezeka kutoka asilimia 78 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 85.3, huku Serikali ikiendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuongeza upatikanaji wa nishati.


Amesema miradi ya nishati safi ya kupikia imeendelea kuongezeka, ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zimeanza kutumia teknolojia hizo na majiko gesi ikiwa miongoni mwa vifaa vilivyosambazwa kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi.


Hata hivyo, ametoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kutekeleza mpango huo kwa kuwa uwekezaji katika nishati safi ya kupikia si suala la kulinda mazingira pekee, bali pia ni fursa ya biashara, uzalishaji na ajira kwa Watanzania.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

UJUE UKWELI KUHUSU JIJI LA MBEYA (GREEN CITY)

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

TIMU YA NGORONGORO KAMA DOUMBIA

KAMISHNA DKT.BADRU ATUA KAMBI YA TIMU YA NGORONGORO KAMA SELEMANI MWALIMU