YONAZI AWATAKA WATAALAMU WA SERIKALI KUJIANDAA KITEKNOLOJIA KUTEKELEZA DIRA YA 2050


NA THADEI HAFIGWA, MOROGORO

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amewataka wakurugenzi wa mipango na wakuu wa idara za Ufuatiliaji na Tathmini katika taasisi za umma kujiimarisha kitaaluma na kiteknolojia ili kuhakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 unazingatia ushahidi, ufanisi na matokeo yanayotarajiwa.


Dkt. Yonazi ametoa wito huo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya kimkakati ya uongozi katika Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya kuimarisha utawala unaotegemea ushahidi, yaliyowashirikisha Wakurugenzi wa Mipango na Wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara pamoja na Sekretarieti za Mikoa.


Amesema wataalamu hao wana jukumu muhimu katika kuhakikisha mipango, sera na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inafuatiliwa na kutathminiwa kwa ufanisi ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho kwa maslahi ya wananchi.


Alisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unahitaji wataalamu wenye uwezo, maarifa na mikakati madhubuti inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya maendeleo ya taifa.


Akizungumzia matumizi ya teknolojia, hususan Akili Unde (AI), Dkt. Yonazi aliwaonya wakurugenzi hao dhidi ya kuitumia teknolojia hiyo kama mbadala wa utaalamu na majukumu ya watumishi, akieleza kuwa inapaswa kuwa nyenzo ya kuongeza ufanisi, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Alisema matumizi ya Akili Unde yanapaswa kuzingatia uhakiki wa taarifa, usalama wa data, uadilifu na viwango vya kitaalamu ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.


Aidha, alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha Mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini, ikiwamo kuweka miundo ya kitaasisi, kuandaa miongozo na kujenga uwezo wa watumishi katika Wizara, Idara na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Hata hivyo, alibainisha kuwa mafanikio ya mfumo huo hayapaswi kupimwa kwa wingi wa taarifa zinazokusanywa pekee, bali kwa kiwango ambacho ushahidi unaozalishwa unatumika kuboresha maamuzi, sera na utekelezaji wa majukumu ya Serikali.


Alieleza kuwa wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini hawapaswi kujikita katika kuandaa taarifa za utekelezaji kwa ajili ya kuripoti pekee, bali wanapaswa kusaidia viongozi kubaini changamoto, kuchambua sababu za matokeo yaliyopatikana na kupendekeza hatua stahiki za kuboresha utendaji.


Katika hatua nyingine, Dkt. Yonazi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Wakurugenzi wa Mipango na Wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini, akieleza kuwa majukumu yao yanategemeana na yanapaswa kuzingatiwa katika hatua zote za maandalizi ya mipango, upangaji wa bajeti na utekelezaji wa shughuli za Serikali.


Alisema mfumo madhubuti wa Ufuatiliaji na Tathmini unahitaji mipango yenye malengo, matokeo na viashiria vinavyoeleweka ili kuwezesha kupima mafanikio kwa usahihi.


Aliongeza kuwa viashiria vya utendaji havipaswi kujikita katika kupima idadi ya shughuli zilizotekelezwa au huduma zilizotolewa pekee, bali pia vinapaswa kuonyesha matokeo na mabadiliko yaliyokusudiwa katika jamii.


Kuhusu ubora wa taarifa, alisema taarifa zinazozalishwa na mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini zinapaswa kuwa sahihi, za kuaminika na kupatikana kwa wakati ili kusaidia viongozi kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kiutendaji.


Aidha, alisisitiza kuwa tathmini za sera, programu na miradi ya maendeleo zinapaswa kulenga kujibu maswali muhimu kuhusu utekelezaji wake na kubaini iwapo malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa, badala ya kufanyika kwa lengo la kutimiza matakwa ya kiutaratibu.


Alionya kuwa mapendekezo yanayotokana na tathmini yanapaswa kufuatiliwa na kutekelezwa, akieleza kuwa tathmini isiyozaa hatua za maboresho hupunguza thamani ya uwekezaji unaofanyika katika mchakato huo.


Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), aliwataka watendaji kutumia mifumo hiyo kuimarisha usimamizi, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa pamoja na kuboresha muunganiko wa mifumo ya Serikali ili kupunguza urudufu wa ukusanyaji wa taarifa.


Alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuongeza uwezo wa viongozi na wataalamu katika Ufuatiliaji, Tathmini, Utafiti na Ujifunzaji (MERL), kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa utendaji wa Serikali unaozingatia ushahidi na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanachangia matokeo bora ya maendeleo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

UJUE UKWELI KUHUSU JIJI LA MBEYA (GREEN CITY)

MAELFU WAFURIKA TIKTOK LIVE YA DHARURA YA WAZIRI GWAJIMA KUHUSU CHANGAMOTO ZA WANAUME KWENYE NDOA

KAMISHNA DKT.BADRU ATUA KAMBI YA TIMU YA NGORONGORO KAMA SELEMANI MWALIMU

TIMU YA NGORONGORO KAMA DOUMBIA