Madereva walia mawaziri kuwatumikisha kama 'punda'

BAADHI ya madereva wa mawaziri na naibu wao wamewashutumu mabosi wao kwa kuwatumia zaidi kama wafanyakazi wa nyumbani, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.
Madereva hao pia wamelalamikia magari ya serikali kutumika vibaya ,kinyume na taratibu za kazi.Baadhi yao waliozungumza na Mwananchi kwa maombi ya kutotajwa majina walidai kuwa, wamekuwa wakifanyishwa shughuli kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane kwa wiki nzima, katika mambo ambayo si ya kiofisi.
"Tunaomba matumizi sahihi ya gari la serikali yazingatiwe na maslahi ya madereva yaangaliwe kwa kina kwa kuwa, tunafanya kazi saa nyingi na kipato ni duni hususan kwa madereva wa mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi," alisema mmoja wa madereva hao na kuongeza:"Hatuna mapumziko, wala sikukuu. Kila siku tupo kazini kwa kuwa waziri anapojisikia kukutuma hata kama ni shughuli yake ya nyumbani, anafanya atakavyo na huwezi kumkatalia."
Waliongeza kuwa kutokana na kutumika hivyo kwa kuwatii mabosi wao na kuwafanyia shughuli kwa matakwa yao, wamekuwa wakikosa hata nafasi ya kukaa na familia zao kama inavyostahili.Walidai kuwa kipato chao ni cha chini, lakini hukitumia kufanyia usafi na kuyatunza magari hayo yaliyonunuliwa kwa gharama kubwa na serikali, lakini watunzaji hao hawathaminiwi.
Walisema kuwa mshahara wao hauzidi Sh 200,000 wakieleza kuwa ajira yao iko katika 'Operation Service' jambo
ambalo linawafanya washindwe kuwa na kiwango cha mshahara kinachowawezesha kukopa kiasi cha fedha ambacho kingewawezesha kuanzisha mradi wowote wa kujiendeleza.
Kufuatia hali hiyo, wameiomba Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kushughulikia tatizo hilo na kuangalia maslahi yao kutokana na kazi wanazozifanya.
Pia, wamemwomba Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka kuangalia suala la wao kuwekwa kwenye 'Operation Service' kwa muda mrefu huku kazi wanazozifanya ni kubwa.
Alipotafutwa jana ili kuzungumzia tatizo hilo, Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi alisema kuwa utaratibu wa mwajiriwa yeyote wa utumishi wa umma uko wazi katika kila wizara akiwataka kuwasilisha malalamiko yao sehemu husika.
Alisema kuwa iwapo dereva ni wa waziri, anajua taratibu zake na kusisitiza kuwa iwapo kuna tatizo, basi liwasilishwe mahali panapostahili."Utaratibu uko wazi na taratibu zote za malalamiko zinafahamika, wakija kulalamika huko kwenu washaurini wafuate taratibu zilizopo,"alisema Yambesi.
Yambesi alisema kuwa ni muhimu kwao (madereva) wawasilishe matatizo yao kwa utaratibu unaofaa, kama si kwa wizara husika, basi wayawasilishe Utumishi ili yaweze kutatuliwa."Wafuate utaratibu wa malalamiko na kazi ya dereva yeyote inajulikana hata kwenye mikataba yetu ya huduma kwa wateja tumeeleza na iko wazi,"alisema Yambesi.
Imedaiwa kuwa mawaziri hao wamekuwa wakitumia magari hayo kwenda kwenye starehe ikiwemo baa na kuwaacha madereva wao wakiwasubiri kwa muda mrefu wanaostarehe, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za serikali.
Magari hayo ya serikali pia yanadaiwa kutumika kwa shughuli binafsi zikiwamo za kuendea shambani, kufuatilia ujenzi wa nyumba, kupelekea watoto shule, pamoja na kwenda kanisani au msikitini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.