MAKATIBU 6 WA MIKOA WAONDOLEWA CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewaondoa makatibu wake wa mikoa zaidi ya sita nchini ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wake wa kujivua gamba ulioanzishwa mapema mwaka huu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wahariri wa magazeti ya kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alipofanya ziara katika makao makuu ya kampuni hiyo Tabata-Relini jijini Dar es Salaam.
MCL ndiyo inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.Katika ziara hiyo, Nape alisema kuwa zoezi hilo la kuwaondoa makatibu litaendelea hadi ngazi ya makatibu wa wilaya ikiwa ni sehemu ya falsafa ya CCM ya kujivua gamba.
Alisema kujivua gamba ni dhana pana ambayo msingi wake ni kufanya mabadiliko ya kiutendaji na uendeshaji wa CCM kwa ujumla wake na kwamba yapo mambo mengi ambayo yamefanywa katika kutekeleza azma hiyo.
“Makatibu wa mikoa kama sita au saba hivi wameshaondoka na wengine wamestaafu, ni katika kujivua gamba na tutaenda kwenye wilaya pia,”alisema Nape.
Alipoulizwa iwapo hao walioondoka katika nyadhifa zao wamestaafu au wameondolewa, Nape alijibu kwa kifupi “vyote kwa pamoja”.
Alitaja baadhi ya mikoa ambayo makatibu wake wameondolewa kuwa ni pamoja na Shinyanga, Dodoma na Kagera.
Utaratibu wa kumpata mgombea uraisAlisema jambo jingine ambalo linafanyika kupitia mchakato huo ni chama hicho kuangalia upya utaratibu wa kumpata mgombea urais ambao utakuwa tofauti na uliokuwa ukitumika katika chaguzi zilizopita.
“Kuna kamati inashughulikia hilo,” Nape alisema na kuongeza:"Pia tunataka tuwe na kamati kama za Bunge ili kutathimini jinsi Serikali inavyotekeleza ahadi ambazo chama kimezitoa ama kupitia wagombea au kwenye Ilani ya Uchaguzi."
Alisema hatua hiyo itakiwezesha chama hicho kubaini udhaifu uliopo katika utekelezaji wa wajibu wake kwa umma, tofauti na sasa ambapo hakuna mfumo unaowawezesha ufuatiliaji huo.
Nape alisema kuwa hivi sasa wanafanya mabadiliko katika mfumo wa uongozi katika makao makuu ya chama hicho na ndiyo maana hakuna mawaziri katika safu za juu za uongozi.
"Hivi sasa hakuna mawaziri, kwani wakati ule walikuwepo mawaziri katika chama ambao ni viongozi, sasa tupo wenyewe na tunakiendesha chama,"alisema na kuongeza:"Hata mfumo wa ndani katika kitengo changu cha Itikadi na Uenezi nako tunafanya mabadiliko na taarifa zitakuwa zikitolewa in details(kwa undani) na si kwa ufupi ili wananchi wazipate."
Kauli yake kuhusu watuhumiwa ufisadiKuhusu watuhumiwa wa ufisadi na siku 90 walizopewa kujiondoa kwenye nyadhifa wanazoshikilia ndani ya chama, Nape alisema kuwa hakuna suala la siku 90 bali ni vikao vya chama vitakutana na kutoa maamuzi.
"Siku 90 zinazozungumzwa ni tafsiri ya watu pale mwenyekiti wa chama (Jakaya Kikwete) aliposema tutakutana baada ya miezi mitatu na watu wakatafsiri hivyo, lakini vikao vya NEC ndivyo vinatoa maamuzi,"alisema Nape.
Alisema kuwa hadi hivi sasa hajui makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa alichozungumza na watuhumiwa hao wa ufisadi baada ya kukutana nao.
"Sikuwepo kwenye kikao hivyo hadi sasa sijui walizungumza nini, na siwezi kwenda kumtaka Katibu Mkuu anieleze kilichozungumzwa kwani katika vikao vijavyo tutapata taarifa,"alisema Nape.
CCM na vijanaNape ambaye alizungumzia mambo mbalimbali ya chama na Serikali alisema kuwa hali ya CCM kuwasahau vijana iliwaletea matatizo katika Uchaguzi Mkuu uliopita na ndiyo maana hivi sasa chama hicho kimeamua kujivua gamba.
Aliwaasa vijana walioko vyuoni kwa sasa akisema kuwa siyo vizuri kwao kudhani kuwa siasa ni ajira na kwamba endapo kila mwanafunzi atafikiria hivyo, hali hiyo haitawasaidia kitu.
Kuhusu takwimu za Serikali na ndani ya CCM, Nape alisema kuwa kuna ugonjwa mkubwa katika utoaji takwimu kwa kuwa takwimu nyingi zimekuwa ni za uongo.
“Udanganyifu wa takwimu unakuwa kama ni tabia na ipo kwenye chama na kwa Serikali,”alisema.
Alisema katika kila jimbo takwimu zao zinaonyesha asilimia 70 hadi 80 ya watu ni wanaCCM, lakini inashangaza kwa nini wanapata ushindi wa chini kwenye uchaguzi.
Wananchi wana haki ya kupata habariAlisema kuwa atakuwa tayari kuwasaidia wanahabari kupata taarifa za serikalini ambazo zinakaliwa na maafisa habari au watu wa serikalini kwa kuwa wananchi wana haki ya kupata taarifa kuhusu Serikali yao.
“Kama kuna taarifa mnaihitaji serikalini nitawasaidia kuipata ili watu wapate habari kwa kuwa, Serikali ni ya CCM na sisi ndiyo viongozi wa chama,”alisema Nape.
Kuhusu kusherehekea miaka 50 ya Uhuru, Nape alisema kuwa ni vizuri wananchi na wanasiasa wakalinda historia ya taifa kwa kuwa limetoka mbali tangu Uhuru ulipotikana.
“Ombi langu kwa wananchi ni hili, miaka 50 ya Uhuru ni safari ndefu, nataka dhana ya kwamba hakijafanyika chochote iondoke, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzia jengo la Ushirika na leo kipo eneo lake halafu mtu anabeza, hilo haiwezekani,”alisema.
Alisema kuwa pamoja na vyombo vya habari kufichua maovu ndani ya nchi, lakini ni lazima vilinde historia ya nchi tangu ilipopata Uhuru.
Akingia kifua gazeti la Mwananchi
Akizungumzia hali ya CCM na Serikali dhidi ya gazeti hili , Nape alisema kuwa fikra ya kwamba chama chake kinaliona gazeti la Mwananchi kama lina mlengo wa chama kingine haipo na ifutike.
“Nimekuja kwa mambo matatu, kufahamiana, kufuta dhana ya CCM kulalamikia magazeti na kutoa msimamo wa chama kuondoa dhana kwamba Mwananchi ina mlengo wa chama kimoja cha siasa,”alisema.
Alisema kuwa ni muhumu CCM ikatambua kuwa gazeti la Mwananchi ni wadau wa mabadiliko katika jamii, hivyo mstari uliopo kati ya CCM na Mwananchi ufutwe.
“CCM kama taasisi tunajua Mwananchi inaaminika na ina wasomaji wengi kuliko gazeti jingine nchini, pia tunajua linaaminiwa na watu na chama pia,” alisema Nape.
Akizungumza kuhusu hilo, Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya MCL, Theophil Makunga alisema kuwa Mwananchi kama gazeti lina sera zake na moja ya sera hizo ni kutoegemea upande mmoja.
Alisema kuwa maamuzi ya habari gani inayofaa kuchapwa kwenye magazeti ya MCL hayafanywi na mtu mmoja bali hupitia vikao vya wahariri vinavyofanyika mara mbili kwa siku.
“Hata editorial (tahariri) haifanywi na mtu mmoja ni uamuzi wa wahariri,”alisema Makunga.
Add this page to your favorite Social Bookmarking websites

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.