ICC: Kenyatta, Ruto wana kesi ya kujibu

NI KUHUSU MACHAFUKO YA UCHAGUZI MKUU 2007, NAFASI YAO YA KUWANIA URAIS SHAKANI, RAIS KIBAKI ANENA
Waandishi Wetu
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iliyoko The Hague, Uholanzi imewakuta na kesi ya kujibu watuhumiwa wanne kati ya sita walioshtakiwa kwa tuhuma za kuhusika katika machafuko yaliyoikumba Kenya wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2007.Waziri wa Fedha na Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura na Mtangazaji wa Redio, Joshua Arap Sang watalazimika kujibu tuhuma zinazowakabili.
Akisoma uamuzi huo mbele ya jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Ekaterina Trendafilova aliwataja watuhumiwa walioachiwa huru na mahakama hiyo kuwa ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Henry Kosgey na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali Hussein Ali.
Uamuzi huo wa awali wa kesi ya watuhumiwa hao sita ambao ni maarufu kama Ocampo Six, ulitangazwa jana moja kwa moja kupitia vyombo vya habari, kutoka katika mahakama hiyo iliyopo mjini The Hague.
Hatua hiyo inaonekana kuwa pigo kubwa kisiasa kwa Kenyatta na Ruto. Waziri huyo wa Fedha, tayari alitangaza nia ya kuwania urais kupitia chama chake cha KANU mwaka huu na Ruto ameshatangaza dhamira ya kuwania ukuu huo wa nchi kwa chama ambacho atajiunga nacho baadaye.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, Ruto alikuwa kambi moja ya chama cha ODM na Waziri Mkuu wa sasa, Raila Odinga na Mbunge wa Mombasa, Najib Balala, Mbunge wa Sabatia, Musalia Mudavadi na Waziri wa Ushirika na Maendeleo ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Gachoka, Joseph Nyaga. Lakini kundi hilo la watu watano lililofahamika kama The Pentagon lilisambaratika.
Katika vurugu hizo, watu 1,300 waliripotiwa kupoteza maisha na wengine zaidi ya 500,000 wakapoteza makazi.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo tangu mwaka jana na pande zote mbili; utetezi na mashtaka zilipata fursa ya kuwasilisha maelezo yao kabla ya uamuzi huo wa jana.Katika shtaka la kwanza, Ruto, Kosgey na Arap Sang, wanatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuwatesa na kuwahamisha watu kwa nguvu.
Uhalifu huo unadaiwa kutekelezwa dhidi ya wafuasi wa chama cha Rais Mwai Kibaki cha Party of National Unity (PNU), katika maeneo kadhaa Mkoa wa Rift Valley.
Katika shtaka la pili, Kenyatta, Muthaura na Jenerali Ali nao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, ubakaji na mateso.Ghasia zilizuka baada ya Rais Kibaki kutangazwa mshindi kwenye uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali kati yake na Odinga.
Kutokana na ghasia hizo, jamii ya kimataifa iliwashinikiza Kibaki na Odinga kufanya mazungumzo kumaliza tofauti zao na kurejesha amani nchini humo.
Mchakato wa usuluhishi uliosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ndiyo uliowezesha viongozi hao wawili kukubali kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa inayoongoza Kenya hadi sasa. Katika mchakato huo, Rais Jakaya Kikwete pia alitoa mchango mkubwa.
Kibaki: Mahakama za Kenya sasa zinaweza
Muda mfupi baada ya kumalizika kusomwa hukumu hiyo, Rais Kibaki alilihutubia Taifa na kumtaka Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo kuipitia hukumu hiyo ya awali kabla kesi ya msingi haijaanza kusikilizwa.
Ingawa hakusema moja kwa moja kwamba kesi hiyo irejeshwe Kenya, Rais Kibaki alisema baada ya vurugu hizo za Uchaguzi Mkuu, Kenya imepitia michakato mbalimbali ikiwamo marekebisho ya Katiba ambayo imebadilisha mfumo mzima wa uendeshaji mashtaka na jeshi la polisi.
“Mahakama zetu sasa zina uwezo wa kuziendesha kesi hizo na kutenda haki hasa baada ya marekebisho ya katiba yetu,” alisema Kibaki.
Ruto, Arap Sang kukata rufaa
Baada ya kutoka kizimbani, Ruto aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema kwamba ataka rufaa kupinga uamuzi huo.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Arap Sang ambaye alisema uamuzi huo si sahihi akisisitiza kwamba hakuhusika wa machafuko hayo ya 2007.Habari hii imeandikwa na Hussein Issa na Daniel Mwingira kwa msaada wa vyombo vya habari vya kimataifa.
 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA