MACHIMBO YA KIWIRA YAUZWA TENA

SERIKALI imeingia tena katika kashfa ya ufisadi wa matumizi mabaya ya rasilimali za umma, baada ya kubainika kuuza kinyemela sehemu yenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe Kiwira kwa kampuni ya Tan-Power Resources (TPR).

Uamuzi huo unaelezwa na wachunguzi wa mambo kuwa utaathiri mradi wa kuzalisha umeme wa makaa ya mawe kwa kusababisha bei ya nishati itakayozalishwa eneo hilo kuwa ghali na italisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 600 milioni sawa na Sh960 bilioni.

Tuhuma hizo za ufisadi, ziliibuka kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na kuifanya iwaite maofisa wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini kujieleza mbele yao, jana.

Sehemu inayodaiwa kuuzwa ilitajwa kuwa ni mlima Kabulo, ambayo aliielezea kuwa ina utajiri mkubwa zaidi wa makaa ya mawe kuliko eneo jingine la Kiwira.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alithibitisha kamati yake kuwaweka 'kitimoto' maofisa waandamizi wa wizara hiyo.

"Tumewaita ili watupe maelezo ya kina kuhusu suala hilo," alisema Zitto akilalamika; "Hili ni tatizo la kuchezea raslimali za nchi,"

Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni alisema tukio hilo limekuja wakati ambao serikali imetakiwa kumiliki hisa zote za mradi huo ili kuhakikisha anapatikana mbia anayeweza kuendesha mradi huo kwa faida.

Alisema mradi huo ambao ulikuwa unamililikiwa kwa pamoja kati ya serikali na kampuni ya Tan-Power Resourses, ulitakiwa kusimamishwa pia wafanyakazi walipwe haki zao.

Lakini mpaka sasa, alisema wafanyakazi hawajalipwa ingawa mradi huo umesimama jambo ambalo linaendelea kuisababishia hasara serikali.

Akizungumzia athari za kuuzwa kwa eneo lenye utajiri mkubwa wa makaa ya mawe, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alisema mradi wa umeme unaotarajia kuanzishwa, gharama yake itakuwa kubwa kutokana na malighafi kuzalishwa na kampuni nyingine.

Ole Sendeka alisema Serikali ilikopa Benki ya Dunia dola za Marekani 600 milioni sawa na Sh960 bilioni kwa ajili ya kuendeleza mradi huo lakini kwa kuuzwa sehemu ya Kiwira, serikali itapata hasara kwa kulipa fedha hizo na riba yake kwa mradi ambao unamilikiwa na kampuni binafsi.

Hadi jana jioni Mwananchi lilipoondoka katika ofisi za Bunge, watendaji wa Wizara walikuwa bado hawajawasilisha maelezo yao mbele ya kamati hiyo.

Historia ya Kiwira

Kiwira ni moja ya miradi ambayo Serikali imeiweka katika orodha ya kuzalisha umeme ili kuliokoa taifa kwenye uhaba mkubwa wanishati ya umeme.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwahi kuliambia bunge kuwa Serikali imeamua kubeba mzigo wa mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ili kuhakikisha kuwa unaleta tija kwa Taifa.

Kampuni ya TPR inadaiwa kumilikiwa na familia ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wa zamani Nishati na Madini, Daniel Yona.

Ngeleja alikuwa ameliambia bunge kuwa baada ya uamuzi huo, serikali imeanza mchakato wa kupata uratatibu muafaka wa kuendesha mradi huo kama ilivyokusudiwa kwa kuangalia fursa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingia mkataba wa uendeshaji na kampuni itakayopewa mamlaka ya kujenga na kuuendesha.

"Chini ya mkataba wa uendeshaji, mkandarasi atapewa jukumu la kujenga uwezo wa mashirika ya Stamico (Shirika la Madini) na Tanesco ili kuyawezesha kumiliki na kusimamia mradi huo," alisema.

Kwa mujibu wa Ngeleja, hatua ya awali ya mpango wa serikali kuanza kuundesha mradi huo zilikuwa zimeanza kwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi waliopo wanalipwa haki zao zote na kuwawekea mazingira mazuri ya kuendelea na kazi.

"Serikali pia imezungumza na serikali rafiki ya China iliyoanzisha na kuendesha mradi huo ili kupata mkopo wa kuufufua na kuhakikisha mradi wa kuzalisha umeme wa MW 200 unakamilika mapema iwezekanavyo," alisema

Akizungumzia suala la Rais Mstaafu Mkapa ambaye aliomba kumiliki hisa 200,000, kupitia kampuni yake ya ANBEN Limited, Ngeleja alisema kuwa kiongozi huyo wa zamani alinyang’anywa hisa hizo Januari 10 mwaka 2005 baada ya kushindwa kuzilipia.

"Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Januari, 2005, (Siku 13 tangu kuanzishwa kwa TPR), ANBEN Limited iliondolewa kuwa miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa TPR.

Hivyo wamiliki wa TPR waliobaki walikuwa ni DevConsult International Ltd, Universal Technologies Ltd, Choice Industries Ltd na Fosnik Enterprises Ltd zote zikiwa na hisa 200,000," alisema Ngeleja.

Wakati huo huo, Zitto alisema jana waliwahoji maofisa waandamizi wa Wizara ya Uchukuzi kwa kile kilichodaiwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuingia kwenye mikataba inayoliingizia taifa hasara.

Zitto hakutaja mambo yaliyofanywa na ATCL na kuisababishia hasara serikali lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa linatakiwa kuilipa kampuni ya kigeni dola za Marekani 36 milioni.

Fedha hizo zinadaiwa kuwa zilitolewa kwa ajili ya kukodisha ndege ambayo hata hivyo haikuwahi kufanya kazi nchini.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA