MAGUFULI ASHITAKIWA KWA PINDA

Waandishi wetu
MBUNGE wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile jana aliwasilisha barua kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa lengo la kupinga ongezeko la nauli ya Kivuko cha Kigamboni.

Akizungumza Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema ameamua kufikia uamuzi huo kwa kuwa ongezeko hilo la nauli lililofanywa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ni batili kutokana na kufanyika kinyume cha taratibu za upandishaji wa nauli za usafirishaji.

Alisema ongezeko la nauli ya Kivuko cha Kigamboni ni batili kutokana na kutoshirikishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) pamoja na wadau mbalimbali.

“Sumatra ndiyo mamlaka husika ya hapa nchini inayotambulika kusimamia masuala ya usafirishaji lakini leo hii nauli za kivuko zimepanda bila Sumatra kutambua kuwa ni utaratibu gani umetumika katika kupandisha nauli hizo. Ni jambo la kushangaza,” alisema Dk Ndugulile na kuongeza;

“Kama Serikali iliweza kuamua kuunda mamlaka kama Sumatra ni lazima kuishirikisha katika mambo mengine ikiwa ni mamlaka ambayo imeipatia majukumu ya kusimamia shughuli zote za usafirishaji nchini.”

Dk Ndugulile alisema kama Serikali imeamua kupandisha nauli, lazima ingewashirikisha wadau wa masuala ya usafirishaji kwa kukusanya maoni na kuweza kutambua hatima yake.

“Naamini Serikali ilikuwa na wazo la kupandisha nauli muda mrefu kwa maana hiyo wangeweza kutumia muda uliopo kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo na mamlaka za usafirishaji ili waweze kuamuru kuhusiana na mkakati wao,” alisema.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Sumatra, David Mziray alisema hawakushirikishwa katika upangaji huo wa nauli kwa sababu sheria inairuhusu Serikali kupanga nauli za vivuko vyake vyote.
Lakini, Dk Ndugulile alizidi kumkaba koo Dk Magufuli akisema  leo wanatarajia kuwasilisha barua ofisi ya waziri huyo kwa lengo kutaka aombe radhi kutokana na kauli zake.

Majuzi, Dk Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika eneo la vivuko hivyo na kuwaambia wananchi waliomzomea kwamba kama wakishindwa kulipa nauli hiyo ya Sh200 ni vyema wakapiga mbizi baharini au kuzunguka Kongowe kuingia katikati ya jiji au warudi vijijini wakalime.

“Nimepokea taarifa kutoka katika vyanzo vya habari mbalimbali kuwa Waziri Magufuli amekataa kuomba radhi kuhusiana na kauli zake alizotoa akidai kuwa hajapata barua ya kumuhusu kuomba radhi. Kwa kuwa ametamka hivyo, uongozi wa wabunge kesho (leo) utawasilisha barua hiyo ili waziri huyo aweze kuwaomba radhi kuhusiana na kauli yake.”

Magufuli apata watetezi
Dk Magufuli ameanza kupata watetezi baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji kuwajia juu wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam akiwataka kuacha kumshambulia waziri huyo  badala yake wahangaike kutatua matatizo ya msingi ya wananchi katika majimbo yao.

Alisema wabunge hawapaswi kupinga kila jambo kwa lengo la kujijenga kisiasa na kusisitiza kuwa, Waziri huyo ana hoja za msingi, hivyo aungwe mkono kwa lengo la kuboresha usafiri wa majini katika eneo hilo na jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi.

“Jamani, ongezeko la Sh100 linaleta chokochoko za nini? Leo hii hata ombaomba ukimpa Sh100 anaweza kukurushia usoni, nadhani wabunge wa Dar es Salaam walipaswa kuunga mkono kwa dhamira kuwa, kivuko kijiendeshe na kutoa huduma za kudumu, badala ya kila kitu kutegemea kitoke Serikali ku.

Mtetezi mwingine ni mkazi wa Makoka, Dar es Salaam, Vicent Michael ambaye amehoji mantiki ya wabunge hao kulalamikia nyongeza ya Sh100 kwenye Kivuko cha Kigamboni wakati wenyewe walisherehekea nyongeza ya Sh200,000 kwenye posho zao za vikao vya Bunge.

“hivi ni kutufanya sisi (wananchi) wapumbavu au vipi? Ni nani asiyejua kama huu ni unafiki. Inaingiaje akilini kuona mtu anasherehekea nyongeza ya Sh200,000 halafu anaandamana kupinga ongezeko la Sh100 kwenye huduma ya umma?”

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA