MBUNGE GALINOMA KUZIKWA LEO ,AACHA WOSIA MZITO KWA TAIFA



WAKATI mazishi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kalenga kati ya mwaka 1995-2000 na 2005-2010 Marehemu Steven Galinoma (79)(CCM) yanataraji kufanyika leo mchana katika kitongoji cha Igawa kijijini kwake Kalenga wilaya ya Iringa vijijini mkoani Iringa siri nzito yafichuka juu ya wosia alioacha marehemu kwa chama cha mapinduzi (CCM) na serikali ya Rais Jakaya Kikwete .

Familia ya marehemu huyo na wazee maarufu wa kijiji cha Kalenga waliyasema hayo katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha Radio Country Fm (88.5) Iringa kuhusiana na kifo cha mbunge huyo na kauli zake za mwisho kabla ya kifo chake.

Mzee Magorosa Mgongolwa (82) alisema kuwa marehemu Galinoma pamoja na kustaafu ubunge bado alikuwa ni kiongozi wa mfano ambaye alipenda kukutana na wananchi wake hasa wazee wa kijiji cha Kalenga na kuwaeleza mambo mbali mbali ya kisiasa na kiserikali .

Alisema mzee Mgongolwa kuwa moja kati ya wosia mzito alioacha marehemu Galinoma ni juu ya mwenendo wa chama chake CCM na kuwa kinapaswa kujirekebisha kwa kuwafukuza mafisadi ndani ya chama hicho ili kukiwezesha kuendelea kufanya vizuri katika chaguzi zijazo .

Kwani alisema kuwa wakati wote Galinoma alikuwa ni mtu wa kusikitika na hali halisi ya CCM ya sasa na kuwa alipenda sana kukutana na viongozi wa juu wa CCM ili kuwapa maoni yake ya jinsi ya kuendesha chama hicho .

Mzee Mgongolwa alisema kuwa pia Galinoma alikuwa hapendezwi hata kidogo na vitendo vya ufisadi vinavyoendelea nchini bila ya kukemewa na wahusika kufilisiwa mali zao.

Kwani alikuwa akipendekeza kuwa viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi wasifikishwe mahakamani kabla ya mali zao kutaifishwa kwa faida ya taifa na kufukuzwa kazi badala ya kuwapeleka mahakamani ambako wamekuwa wakishinda kesi na kuzidi kuliingiza taifa katika hasara kubwa ya uendeshaji wa kesi hiyo .

Hivyo alisema kuwa wakati Taifa linaomboleza kifo cha mbunge huyo lina kila sababu ya kutekeleza wosia wake huo kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kukifanya chama hicho tawala kuwa chama cha wanyonge badala ya kuwa chama cha matajiri na wenye uwezo.

Kwa upande wake mtoto mkubwa wa marehemu Galinoma Magreth Galinoma alisema kuwa babake muda wote alikuwa ni mtu wa kusikitika na hali ya kisiasa nchini na vitendo hivyo vya ufisadi japo alisema angeweza kuweka wazi katika vyombo vya habari jinsi nchi inavyo kwenda ila kifo chake kilimfanya asifanye hivyo.

Mjane wa marehemu Ameria Galinoma alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa ratiba ya mazishi itaanza mida ya saa 7 mchana kwa ibada itakayofanyika katika kanisa la RC Tosamaganga na baada ya hapo mwili utasafirishwa hadi makabuli ya Igawa Kalenga kwa mazishi .

Hata hivyo alisema hadi jana saa 8 mchana wakati habari hii inakwenda mtamboni bado walikuwa hawajapata taarifa ya mgeni atakayeongoza mazishi hayo japo tayari viongozi mbali mbali wa chama na serikali ngazi ya wilaya hadi mkoa wamepata kufika kutoa mkono wa pole.

mwandishi wa habari hizi alimtafuta kwa njia ya simu mkuu wa mkoa wa Iringa Dr.Christina Ishengoma (MB) ili kujua kama ofisi yake tayari imepata taarifa ya kiongozi yeyote wa kitaifa atakayefika kushiriki mazishi hayo ,amedai bado na kuwa iwapo atapokea taarifa angezitoa .

Wakati huo huo wabunge wa mkoa wa Iringa wametuma salamu za rambi rambi kwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Deo Sanga na familia ya Galinoma kwa kifo cha mbunge huyo .

Mbunge wa jimbo la Ismani Wiliam Lukuvi (CCM) ambaye ni waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge amesema kuwa kifo cha mzee Galinoma ni pigo kubwa kwa wakazi wa jimbo la Kalenga ,mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla na kuwa mchango wake bado ulikuwa ukihitajika katika kipindi hiki.

Lukuvi alisema kuwa katika uhai wake Galinoma akiwa ni mbunge na mwenyekiti wa wabunge wa CCM mkoa wa Iringa alikuwa na msimamo mkali katika kupigania maendeleo ya mkoa wa Iringa .

Hivyo alisema kuwa njia pekee ya kumuenzi Galinoma ni kufanya kazi kwa kujituma zaidi na kuwatumikia wananchi kwa viongozi wa siasa na serikali.

Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) alisema kuwa mbali ya kuwa yeye wakati akiingia madarakani Galinoma alikuwa akistaafu ubunge ila bado jina la Galinoma si geni masikioni na machoni kwa watanzania na kuwa kati ya wabunge waliokuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja bungeni ni pamoja na mzee Galinoma.

Mbunge wa jimbo la Kilolo Prof.Peter Msolla ambaye ni mjumbe wa NEC mkoa wa Iringa alisema kuwa kifo cha Galinoma ni pengo kubwa na kuwa kwa niaba ya wana Kilolo na wana CCM wanaunga na familia yake katika kuomboleza msiba huo mkubwa .

Wabunge wengine waliotuma salamu za rambi rambi ni pamoja na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati (CCM) Lediana Mng'ong'o (CCM) ambao walisema kuwa msiba huo umewashitua sana na kudai kuwa Galinoma atakumbukwa kwa mengi katika taifa hili kutokana na utendaji kazi wake.

Wakati mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi , katibu tawala wa mkoa wa Iringa Getrude Mpaka na mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Ishengoma walisema kuwa kifo cha Galinoma ni pengo katika mkoa wa Iringa .

Mbunge Galinoma alifariki dunia juzi majira ya asubuhi wakati akikimbizwa katika Hospital teule ya wilaya ya Iringa (hospital ya Ipamba) baada ya kuzidiwa ghafla akiwa nyumbani kwake Kalenga .

Kwa mujibu wa Magreth Galinoma alisema kuwa kabla ya kuzidiwa marehemu Galinoma alikuwa akitibiwa katika hospital mbali mbali hapa nchini na nje ya nchi na kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa kansa ya kibofu cha mkojo .

Alisema kuwa siku moja kabla ya kifo chake alifikishwa mjini Iringa katika Hospital ya Aghakan kwa ajili ya kutazamwa afya yake na kupatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani na leo asubuhi aliomba kupewa maziwa na baada ya kupewa maziwa hakuweza kumaliza kikombe kimoja baada ya maziwa hayo kila anapojaribu kunywa kumshinda na kutokea puani na mdomoni na ndipo walipoamua kumkimbiza Hospital ili kusaidiwa zaidi na wakiwa njiani alifariki dunia.

Marehemu Galinoma katika uhai wake alipata kushika nafasi mbali mbali serikalini na katika chama cha mapinduzi (CCM) kwa kuwa mbunge wa jimbo hilo la Kalenga katika vipindi viwili tofauti kuanzia 1995 hadi 2000 na baada ya hapo alishindwa katika kura za maoni na George Mlawa ambaye alipata kuongoza kutoka mwaka 2000 hadi 2005 na baada ya hapo ndipo mzee Galinoma aliposhinda tena kura za maoni na kuongoza toka mwaka 2005 hadi mwaka 2010 na kuamua kustaafu ubunge na nafasi yake kuchukuliwa na mbunge wa sasa Dr Wiliam Mgimwa.

Pia alipata kuwa katibu mkuu wizara ya ulinzi kipindi cha serikali ya awamu ya kwanza ,alipata kuwa mkurugenzi wa bodi ya hifadhi ya Taifa (TANAPA) na nafasi nyingine nyinge katika taifa. Chanzo Blog ya Francis Godwin.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA