MGOGORO WA MADAKTARI WAWAGAWA WABUNGE


MGOMO wa madaktari ambao umekuwa ukitikisa nchi kwa siku kadhaa sasa, jana uliibua mvutano mkubwa ndani ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, wakati wakijadili mgogoro huo ulipo kati ya wanataaluma hao na serikali.

Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata kutoka ndani ya kikao hicho kilichokuwa kikifanyika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, zilisema baadhi ya wabunge hawataki madaktari hao wasikilizwe matatizo yao huku wengine wakitaka wasikilizwe.

Juzi, serikali ilitoa tamko kupitia kwa Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya ambalo pamoja na mambo mengine lilitupilia mbali madai mawili ya madaktari hao huku ikitetea uamuzi wake wa kuwatanya kwenye vituo mbalimbali kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Jana, chanzo chetu cha habari kilifafanua kwamba sakata hilo liliibuka ndani ya kamati hiyo ya Bunge baada ya mmoja wa wabunge kutaka kamati hiyo iwasikilize madaktari hao kitendo ambacho kilipingwa vikali na baadhi ya wabunge wenzake na kufikia hatua ya kutoleana maneno makali.

"Kumekuwa na mvutano, wengine wakitaka madaktari wasilikizwe wengine wakikataa na kutaka serikali iwawajibishe bila kuwasikiliza kitu ambacho kimeleta mtafaruku na kufokeana kwa baadhi ya wabunge,"kilieleza chanzo chetu ndani ya kamati hiyo.

Chanzo hicho kiliongeza: "Kuna mmoja wa wabunge na mwenzake mwingine walisimama na kufoka utafikiri madaktari hawapaswi kusikilizwa na ikafikia hatua, kila mtu akawa anazungumza hivyo kikao kikasitishwa na mwenyekiti."

Kutokana na hali hiyo kikao kilisitishwa bila kufikiwa muafaka huku ikielezwa kuwa katibu wa kamati hiyo ametakiwa awaandikie barua ya kuwaita madaktari hao mbele ya kamati.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, wakati mvutano huo ukitokea Naibu Waziri wa Dk Nkya alikuwa akitoa taarifa yake mbele ya kamati hiyo kuhusu jinsi serikali inavyoushughulikia.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Margaret Sitta alipouluzwa kuhusu suasa hilo alikanusha kuwapo kwa mvutano miongoni mwa wanakamati wake na kwamba kila kitu kilikuwa kikienda sawa.

"Huyo aliyekueleza mwambie akumalizie yote, hakuna kitu kama hicho hivyo tunaendelea na kikao kujadili suala hilo,"alisema Sitta kwa kifupi.

Hawakukutana na Waziri

Katika hatua nyingine madaktari hao jana walishindwa kukutana na Dk Nkya kama ilivyotarajiwa kitendo ambacho kilitokana na pande hizo kutunishiana misuli.

Mkopi alisema hali hiyo ilitokana na kitendo cha Dk Nkya kwenda katika ukumbi mwingine huku akijua kuwa wao walikuwa kwenye ukumbi wa Don Bosco na kwamba ni dhahiri kwamba hakuwa tayari kukutano nao.

Mkopi alisema kwa hali hiyo kama ingewezekana wanachama wanahitaji kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili aweze kuwasikiliza na kuwapa majibu ya uhakika kuhusu madai yao.

Alisema uongozi wa chama hicho mapema jana asubuhi uliwasilisha barua wizarani pamoja na muhitasiri wa kikao huku ikielezea bayana kwamba wapo kwenye ukumbi wa Don Bosco ambao tayari walikuwa wameulipia kwa ajili ya mkutano.

Alisema hali hiyo ilizua mvutano baada ya waziri huyo kutaka uwepo ukumbi mwingine ambao ungeandaliwa na wizara.

"Tulimweleza tunarudi kuwaeleza wanachama wetu nao ndio watakaoamua na tuliporudi tukiwa kwenye chumba cha mkutano tulipigiwa simu na msaidizi wa waziri akidai ukumbi umepatikana Karimjee,"alisema Mkopi.

Alisema wakati wakiendelea kujadili kama wangeenda katika ukumbi huo au la walipewa taarifa kuwa ukumbi umebadilishwa na sasa watakuwa Arnatouglou.

"Tulikataa hilo kwa sababu tatu,tupo hapa zaidi ya 300 tukitoka hapa kwenda Anatouglo tutaonekana tunaandamana na polisi waliopo hapo nje watatushambulia, muda aliotoa tungefika na kukuta ameondoka na tatu sisi ndio wenye mkutano tumeandaa,"alisema Mkopi.

Madaktari hao walisema watakutana kuanzia saa 3:00 asubuhi na kwa lolote litakalotokea wataeleza uamuzi wao.

Mvutano

Juzi Rais wa MAT Mkopi alitaja hoja tatu za msingi zinazohitaji majibu kuwa ni pamoja na mustakabali wa afya ya Mtanzania, unaokwenda sambamba na maboresho ya mafao yao.

Madaktari hao waliitisha mkutano huo kujibu kauli ya serikali iliyotolewa na Dk Nkya dhidi ya madai yao ya awali kuwa hayana msingi.

Alitaja madai yao kuwa ni pamoja pia na kupatiwa nyumba za kuishi, kuongezewa posho za muda wa ziada za kazi ambazo sasa ni Sh 10,000 na mishahara.

Katika tamko la serikali la mapema wiki hii, Dk Nkya alisema tathmini iliyofanywa na wizara ilibaini kuwa idadi ya madaktari waliokuwa katika mafunzo kwenye hospitali ya Muhimbili ni kubwa kuliko uwezo wake akisema wingi wao ungeathiri mafunzo ya taaluma yao.

Dk Nkya alisema uongozi wa hospitali hiyo ulilazimika kuwandikia barua ya kuwarejesha wizarani, kutokana na kitendo chao cha kugoma.

Alisema madaktari hao hawakufukuzwa kazi, bali walirejeshwa wizarani ili kupangiwa vituo vingine vya kazi kumalizia muda wao wa mazoezi kwa vitendo, baada ya kuvunja mkataba na uongozi wa hospitali hiyo.

Januari 2, mwaka huu, madaktari 194 waliokuwa kwenye mazoezi ya vitendo waligoma kufanya kazi wakishinikiza Serikali iwalipe posho zao za miezi miwili zilizokuwa zimecheleweshwa.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.