MNYIKA ACHUKIZWA WANAFUNZI KUFUKUZWA UDSM


Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kufukuzwa kwa wanafunzi 13 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakiwemo viongozi wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) na wengine 86 kusimamishwa masomo kuanzia tarehe 10 Januari 2011.
Kutokana na hali hiyo nakusudia kukutana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufanya mazungumzo ili maamuzi hayo yaweze kubadilishwa na iwapo hatua muafaka. Iwapo ufumbuzi wa mapema hautapatikana pamoja na kuchukua hatua zingine za kibunge nitakazozieleza baadaye nitatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kwa kuwa matatizo katika vyuo vikuu kwa sasa yamechangiwa na udhaifu wa kiutendaji katika Serikali.
Ikumbukwe kwamba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa aliahidi bungeni kwenye mkutano wa nne kwamba serikali imepata mkakati wa kumaliza migogoro na matatizo katika vyuo vikuu nchini na kwamba hatua za haraka zingechukuliwa kama sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/12.
Hata hivyo, badala ya migomo na migogoro kumalizika inaelekea kuongezeka na kufikia kiwango cha wanafunzi kufukuzwa na wengine kusimamishwa katika vyuo vikuu mbalimbali vya umma ikiwemo Chuo Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM),  Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake. Hali katika vyuo vikuu hivi na vingine haiendani na ahadi ambayo Waziri Kawambwa alizitoa bungeni na kwa umma miezi kadhaa iliyopita.
Kutokana na hali hiyo tarehe 12 Desemba 2011  niliwasiliana na wizara yenye dhamana ili iweze kuingilia kati kama sehemu ya kutimiza ahadi iliyotolewa bungeni hata hivyo hatua muafaka hazikuchuliwa.
Katika kukabiliana  migomo na migogoro katika elimu ya juu serikali imekuwa ikichukua hatua dhidi ya matokeo badala ya kushughulikia vyanzo vya matatizo hivyo natarajia wakati huu Waziri husika atajielekeza katika madai ya msingi ya wanafunzi na wahadhiri.
Serikali itambue kwamba chanzo cha migomo ya hivi karibuni UDSM ni kugeuzwa kwa taratibu za utoaji mikopo na hatimaye kuchelewa kwa malipo ya wanafunzi na wengine kupata pungufu au kukosa kabisa. Katika mazingira hayo nasisitiza kwamba ni muhimu kwa Waziri Kawambwa kuweka wazi kwa umma ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Kuwekwa wazi kwa taarifa hii kutawezesha wawakilishi wa wananchi, wanafunzi, wazazi, vyuo vikuu na wadau wengine wote kuunganisha nguvu katika kushughulikia matatizo yanayoendelea kujitokeza katika elimu ya juu hivi sasa.
Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete aliahidi mwaka 2007 kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wanafunzi wa elimu juu nchini ili kupunguza migomo na migogoro. Katika Mkutano wake na wanafunzi wa vyuo vikuu mwezi Februari 2007 alikwenda mbali zaidi kwa kuwaeleza kwamba hakuna mtoto wa maskini atayeshindwa kuendelea na masomo kutokana na masharti ya mikopo.
Miaka mitano imepita toka ahadi hizo zitolewe migomo katika vyuo vikuu inaendelea na pia wapo watoto wa walalahoi ambao wamefaulu kidato cha sita lakini wemeshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo; hivyo Waziri asipochukua hatua za haraka itadhihirika kwamba ahadi za serikali zimekuwa za ‘kiini macho’.
Izingatiwe kuwa kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake.


John Mnyika (Mb)
11/01/2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA