SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS JAKAYA KIKWETE KWA MSIBA WA MBUNGE WA ZAMANI WA KALENGA, STEPHEN GALINOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga kufuatia kifo cha Steven Johns Galinoma aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Kalenga mkoani Iringa kwa tiketi ya CCM.
Marehemu Steven Galinoma amefariki leo tarehe 26 Januari, 2012 saa 4.00 asubuhi akiwa njiani kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Ipamba iliyopo Iringa Vijijini kwa matibabu kutokana na ugonjwa wa saratani akitokea kijijini kwake Kalenga.
Enzi za uhai wake, Marehemu Steven Galinoma pia aliwahi kufanya kazi Serikalini kwa muda mrefu na kushika nyadhfa mbalimbali hadi kufikia wadhfa wa Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Steven Johns Galinoma aliyewatumikia na kuwaongoza kwa uadilifu na uhodari mkubwa wananchi wa Jimbo la Uchaguzi la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.
Aidha Rais Kikwete amesema hata alipokuwa katika utumishi wa Serikali enzi za uhai wake, alimfahamu Marehemu Galinoma kama kiongozi shupavu, mwadilifu na mchapakazi hodari.
Rais Kikwete amemuomba Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia.
“Natambua uchungu mkubwa walio nao kwa kuondokewa na mpendwa wao, lakini nawahakikishia kwamba nipo pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa”, amesema Rais Kikwete na kwamba anamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Steven Galinoma, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
26 Januari, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA