SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA FAMILIA YA ALIYEKUWA MBUNGE WA ARUMERU MASHARIKI, MAREHEMU JEREMIAH SUMARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete  (pichani) amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.,) kutokana na kifo cha Mhe. Jeremia Solomon Sumari, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM na aliyepata kuwa Naibu Waziri, kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 19 Januari, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari kwani alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhfa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete amesema kutokana na kifo chake, wananchi wa Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa sana huku Taifa likiachwa na pengo kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

“Kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia.  Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Jeremia Solomon Sumari mahali pema peponi, Amina”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Ameiomba familia ya Marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

19 Januari, 2012

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA