Serikali yapewa saa 72 kuwarejesha madaktari Muhimbili


Serikali yapewa saa 72 kuwarejesha madaktari Muhimbili
Dk. Mtasiwa asimamishwa uanachama kwa mwaka mmoja
JK atakiwa kuwatafutia kazi nyingine Nyoni, Dk. Mtasiwa.

Na Richard Mwaikenda

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeipa Serikali saa 72, kuwarejesha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wanafunzi waliofuzu udaktari waliondolewa hapo baada ya kugoma wakidai malipo yao.

Tamko hilo lilitolewa na Rais wa chama hicho, Dk Namala Mkopi katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.

Chama hicho kimemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuwatafutia kazi nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa kwa kosa la kumshauri vibaya Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hadji Mponda. Alisema Dk. Mponda anasamehewa kwani hajui alitendalo ila inatakiwa awaombe radhi kwa kuwaita madaktari wenzao kuwa si madaktari bali bado wangali wanafunzi.

Rais wa MAT, Dk. Mkopi, pia alitangaza kuwa kimefutia uanachama kwa mwaka mmoja, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Mtasiwa kwa kosa lake la kuusaliti udaktari kutokana na kukiuka kiapo cha udakatari kinachosema kuwa Madaktari wote ni ndugu na nitawatendea haki kama dada na kaka.

Alisema endapo Dk. Mtasiwa atanendelea na tabia hiyo ya kudharau taaluma ya udakatari, basi chama kitaamua kumfukuza kabisa na kumuweka kwenye mtandao wa madaktari duniani, ili iwe fundisho kwa madaktari wengine wenye tabia hiyo.

Dk. Mkopi alisema kuwa chama kimesikitishwa sana na kwamba hawaoni ni kwa nini Serikali imeamua kuwaadhibu madaktari wenzao waliokuwa wakidai haki ya msingi, na kuwaacha kuwaadhibu watu waliosababisha ucheleweshaji wa makusudi wa kutowalipa malipo yao madaktari.

Aliwataka viongozi kuacha tabia ya kutumia siasa kuingilia masuala ya kitaaluma, na kwamba wanavyofanya hivyo, wajue kwamba wanaowakomoa si madaktari bali ni wagonjwa. Alisema kitendo cha kuwaondoa madakari zaidi ya 200 tayari kimeanza kuleta athari kwa madakatari mabingwa waliokuwa wakisaidia kazi, na kwamba kibaya zaidi kusababisha wagonjwa wengi kufariki katika Hospitali hiyo.

Alisema kitendo cha Serikali kuwaondoa madaktari wenzao katika Hospitali ya Muhimbili na kuamua kuwapangia Hospitali zingine si kizuri, kwani baadhi ya hospitali walizohamishiwa hakuna nafasi wala mambo wanayotakiwa kujifunza, hivyo mpaka sasa hakuna wanalolifanya.

Chama hicho, kimeitisha mkutano mkubwa wa madakari wote nchini, Jumatano ijayo utakaofanyika, Dar es Salaam, na kuzungumzia mambo kadhaa likiwemo la madakatari wenzao.

Alitaja baadhi ya ajenda watakazozungumzia kwenye mkutano huo, kuwa ni;Hatima ya heshima ya udaktari, Ulipaji posho kwa madaktari, Mshahara uendane na elimu, majukumu na hadhi ya udaktari, madaktari kupewa nyumba, posho ya mazingira magumu, posho ya mazingira hatarishi pamoja na uhamishaji ovyo wa madaktari.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA