UVCCM YAWAJIA JUU WANAOIVURUGA JUMUIYA HIYO KWA TAMAA YA URAIS 2015

WAAPA KUFA NA WANAOTAKA URAIS KWA KUVURUGA UMOJA HUO, WENZAO CHADEMA WAOMBA MSAADA MATAIFA YA NJE
Fredy Azzah na Keneth Goliama
VITA ya makundi ya urais ndani ya CCM imezidi kukitikisa chama hicho na jumuiya zake, baada ya jana, Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Benno Malisa kusema watapambana na yeyote atakayetaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015 kwa kufanya kampeni chafu za kuuvuruga umoja huo.Onyo hilo la UVCCM limekuja siku moja baada ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu kusema mbio za urais za 2015 zimeliweka taifa njia panda huku akianika wanaotajwa kuutaka ukuu huo wa nchi baada ya Rais Kikwete.
Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa akivishwa mavazi la asili la kabila la Wachagga
Jana, Malisa katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa makatibu wa wilaya na mikoa wa UVCCM uliofanyika Mjini Dodoma, alionya kwamba vijana hawatakubali kuona watu wenye kutaka urais wanavuruga umoja huo kwa maslahi binafsi ya kisiasa.

Kuhusu uchaguzi wa CCM na jumuiya zake utakaofanyika mwaka huu Malisa alisema: “Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu sana katika historia ya chama chetu. Unaweza kutufanya tukaimarika zaidi mbele ya umma wa Watanzania au kutubomoa mbele ya jamii hasa vijana ambao si wanachama wetu lakini tunawahitaji kwa dhati watuunge mkono katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015.”

“Ni matumaini yangu kwamba, uchaguzi huu utaendelea kujenga umoja wetu na kutuweka karibu zaidi na vijana wenzetu kama utafuata taratibu ambazo tumejiwekea na ambazo zinakubalika na Chama chetu Cha Mapinduzi bila kuingiliwa na watu wenye ajenda zao za siri na ambao si wanachama wa jumuiya yetu.”

Malisa ambaye katika siku za karibuni amekuwa akitoa matamshi mazito, aliwataka wanachama wa jumuiya hiyo, kumchagua mtu bila kushinikizwa na yeyote.

“Watu wakipita huko wakiwaambia mchagueni huyu kwa sababu ni wa kundi langu, kataeni, waambieni hapa tunachagua viongozi bora wa kuitumikia jumuiya, chama chetu na taifa letu, hatuchagui kundi la mtu hapa kwa ajili ya maslahi yake binafsi,” alisema Malisa.

Akimnukuu aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair alisema: “Kipaji cha uongozi ni uwezo wa kiongozi kusema hapana na siyo kusema ndiyo. Nukuu hii ya Tony Blair ni muhimu sana katika uchaguzi ndani ya jumuiya yetu. Tunataka watendaji wetu wafuate amri za kanuni zetu ambazo tumejiwekea na si maagizo ya watu fulani ambao malengo yao hatuyajui.”

Kiongozi huyo wa juu wa UVCCM ambaye anamaliza muda wake, aliwataka vijana wa chama hicho kugombea nafasi za chama hicho, lengo likiwa kuwawezesha vijana zaidi ya asilimia 60 kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho.
“Umewadia wakati wa kujitafutia kura wenyewe na si kuwatafutia wengine ni lazima uwakilishi ndani ya chama ufanane na hali halisi ya idadi ya vijana,” alisema Malisa.

Aliwapua mawaziri
Alisema kumekuwepo na utaratibu wa wana CCM mbalimbali huku wengine wakiwa ni mawaziri, kusutana kupitia vyombo vya habari na kwenye mikutano ya hadhara, hali inayokiumiza chama.
Alisema watu wanaofanya hivyo wanapoulizwa, wanajificha nyuma ya vivuli mbalimbali vikiwamo vya kutumia uhuru wao wa kidemokrasia wa kutoa maoni.

“Au wa kuuonyesha umma kwamba wanafanya hivyo kwa nia safi ya kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi vilivyokithiri miongoni mwa jamii, kivuli kikubwa wanachojivalisha ni uzalendo na uzawa,” alisema Malisa.

Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa, ndiyo iliyosababisha nyufa katika jumuiya hiyo, chama na pia kwenye Serikali.
“Bado tunao muda wa kutosha wa kujipanga upya kwa nia ya kusahihisha makosa makubwa ambayo tumeyafanya kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa ndani wa chama, baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” alisema.
Alisema kwa sasa chama hicho kinafanya kazi kubwa ya kudandia na kukumbatia kwa gharama kubwa hoja za vyama vya upinzani pamoja na zile za magazeti, hali aliyosema inakigharimu.

Chadema waomba msaada wa mataifa ya nje
Wakati UVCCM ukitoa mwongozo wake, wenzao wa Chadema (Bavicha) wamekimbilia mataifa ya nje kuomba msaada kwa vyama rafiki ili kufanikisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akihutubia katika Mkutano wa Kimataifa wa Vijana kuhusu demokrasia uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Bunge la Australia (North Wales), Sydney, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratias Munish alisema: “Chadema tumedhamiria kushika dola mwaka 2015, tunaomba msaada wenu wa hali na mali katika harakati zetu hizi.”

Katika hotuba yake, Munishi alisema kutokana na matatizo mengi yanayoikumba Tanzania hasa katika mfumo wa uchaguzi, wameamua kufanya tathmini ya kukiwezesha kuingia Ikulu kwa kuwashirikisha vijana wa nchini nzima.Alisema ili kufanikisha hilo, kinahitaji kupata uzoefu wa nchi mbalimbali kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi.

“Tunahitaji kufanya ‘home work’ yetu vizuri kabla ya hapo. Ndiyo maana kama vijana wa chama, Baraza letu limeamua kwa makusudi kwenda kukijenga chama vizuri kwa kuwaunganisha vijana wote pamoja kwenye maeneo yao,” alisema.
Alisema kabla ya Bavicha kujipanga kuhakikisha Chadema kinashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao, Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa alishaiagiza Bavicha kufuatilia kwa karibu migogoro yote inayohusu vyuo vikuu ambako ndiko iliko ngome kuu ya chama hicho.

Munish alisema Dk Slaa alisema vijana hao wanatakiwa kufuatilia na kuweka wazi hatua mwafaka zinazopaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na matatizo ya vijana.

Alisema uwanja wa siasa nchini ni mchafu kutokana na kuwepo kwa katiba mbovu ambayo pamoja na mambo mengine, inakataza kuhoji matokeo ya urais pindi yatakapotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.Alisema ndiyo maana baraza hilo la vijana limeamua kukijenga chama kwa kuwaunganisha vijana wote pamoja kwenye maeneo yao ili kuhakikisha muungano wa ushindi 2015 unapatikana.

Alisema kutokana na vijana wengi duniani kuunganishwa na misingi ya vyama vyenye kusimamia na kuamini katika demokrasia, jambo la msingi ni kuhakikisha haki za binadamu na uhuru wa kweli unapatikana.

“Ninaamini na nina uhakika mtatuunga mkono katika harakati zetu sisi vijana wa Tanzania katika kuhakikisha tunashinda 2015,” alisema Munishi na kuongeza: “Kukua kwa Chadema si kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na nia na mipango yake thabiti ya kuutumikia umma wa Tanzania.”

Alisema huduma mbovu za kijamii zimekuwa zikififisha ndoto za Watanzania kufikia maendeleo ya kweli hasa katika kipindi hiki cha kudorora kwa uchumi.Alisema kutokana na hali hiyo, Chadema kimeamua kupambana na rushwa bila woga kwa kuwafichua viongozi wala rushwa ambao wamekuwa wakilifilisi taifa kwa vitendo vyao hivyo.

Alisema Chadema na Watanzania hawajakata tamaa na huku akiwataka wajumbe waliohudhuria mkutano huo kuwaunga mkono katika kuendeleza mapambano ya kuongoza umma kueleza maovu yanayotendwa na Serikali.
Nchi wanachama wa umoja huo wenye wanachama 45 inashirikisha vyama vilivyopo madarakani na ambavyo havipo madarakani.

Baadhi ya nchi hizo wanachama ni Albania, Australia, Austria, Colombia, Croatia, Cyprus, Jamhuri ya Czech, Denmark, Ecuador, El Salvador, Finland, Ufaransa, Georgia, Ujerumani na Ghana.Katika orodha hiyo pia vipo vyama kutoka nchi za Ugiriki, Guatemala, Honduras, Hungary, Iceland, Korea Kusini, Macedonia, Maldives, Moldova na Mongolia.
Vingine vinatoka katika nchi za New Zealand, Nicaragua, Norway, Peru, Ureno, Serbia, Slovenia, Hispania, Sri Lanka, Sweden, Uganda, Uingereza, Venezuela, Belarus, Bolivia, Malta, Msumbiji, Namibia, Panama, Russia na Tanzania inayowakilishwa na Chadema.Katika mkutano wa aina hiyo uliofanyika nchini mwishoni mwa mwaka jana, ulihudhuriwa na nchi 24.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA