'UTEJA basi', kauli mbiu ya Taifa Stars leo wakati watakaposhuka kwenye Uwanja wa Taifa kuikabili Msumbiji katika mchezo wa kwanza wa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika 2013.

Stars inashuka dimbani ikiwa na deni kubwa la kufuta uteja dhidi ya Mambaz kwenye uwanja huo baada ya kupoteza mechi mbili muhimu, ikiwemo ya mwaka 2007 iliyoinyia Tanzania fursa ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2008 nchini Ghana.

Wachezaji pekee wa Stars walikuwamo kwenye kikosi hicho ni viungo Nizar Khalfan na Abdi Kassim wanaotegemewa kuwaongoza wenzao kuhakikisha wanaondoka na ushindi leo.
Nizar alisema: "Nafikiri tuna kila sababu ya kushinda mchezo huu, kikubwa kila atakayepata nafasi ya kucheza ajitume na kujitoa kwa ajili ya Taifa lake."

Nizar anarudisha nyuma kumbukumbu iliyowaacha mashabiki wa soka vichwa chini Septemba 2007, wakati mshambuliaji wa Msumbiji, Tico-Tico wa Msumbiji alipofunga bao la kichwa dakika ya kwanza kuinyita Tanzania safari ya Ghana.

Hata hivyo, Tico Tico siyo miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Msumbiji cha sasa kilichojaa nyota wengi wanaocheza soka ya kulipwa Afrika Kusini, Romania na Ureno.
Stars itaingia uwanjani wakiendelea kutumia mfumo wao wa 4-2-3-1 uliowasaidia kupata suruhu dhidi ya DR Congo mwishoni mwa wiki hii.

Mfumo huo ulisaidia ngome ya Stars na kuoneka imara na kutoruhusu kufungwa, lakini viungo wake washambuliaji Hussen Javu, Mrisho Ngasa na Abdi walioneka kushindwa kufuta maelekezo na kushindwa kumsaidia John Boko kwenye umaliziaji.

Uwapo wa Nizar utamfanya Kocha Jan Poulsen kufanya mabadiliko kidogo kwa kumweka benchi Javu ili kutoa nafasi kwa kiungo wa zamani wa Vancouver Whitecaps kusaidiana na Kassim katikati ya uwanja.

Poulsen ambaye mkataba wake utamalizika baada ya mechi ya marudiano dhidi ya Msumbiji mwezi Juni, leo atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anashinda ili kuwashawishi Watanzania kwamba anastahili kuongezewa mkataba.Poulsen alisema ana imani wachezaji wake watapata matokeo mazuri leo kama wakiungwa mkono na Watanzania wote.

"Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yao ili kuwapa moyo wachezaji waweze kufanya vizuri.

“Tunawaomba Watanzania wote kutuunga mkono kwenye mechi yetu ya kesho (leo) ili tufanye vizuri na hatimaye kujiweka kwenye mazingira ya kusonga mbele.“Kwa hakika vijana wapo vizuri na wana morali ya kufanikisha malengo yetu japokuwa siwezi kusema moja kwa moja kama tutashinda mchezo huo,” alisema Poulsen.

Msumbiji watashuka kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa 3-0 na Namibia kwenye mchezo wao wa kirafiki uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kocha Msumbiji, Gert Engels anatarajia kuwaanzisha nyota wake wote wanaocheza soka kulipwa nje ili kupata ushindi ugenini.Alisema kufanya kwake vizuri katika mechi hiyo kutakuwa kumemfungulia njia ya safari yake ya kuelekea Afrika Kusini.

“Nina matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo, japo mchezo wa soka wakati mwingine huwa na matokeo ya ajabu kabisa na vigumu kutabiri,” alisema Engels.

Mechi ya mwisho iliyozikutanisha timu hizo mwaka jana mwezi Aprili 23, kwenye ufunguzi wa Uwanja wa taifa wa Zimpeto, na Mambas ilishinda 2-0 mabao yote yalifungwa mshambuliaji Jerry.

Hii ni mara ya tano kwa Tanzania na Msumbiji kucheza kati ya hizo Mambaz imeshinda mechi mbili na kutoka sare mbili.

Kama Taifa Stars ikifanikiwa kuingia raundi ya pili itacheza mechi moja ugenini na moja nyumbani mwezi Septemba na Oktoba, ambapo timu 15 zitakazoshinda katika hatua hii raundi ya pili zitafuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika 2013.

Mbali ya mchezo huo pia kutakuwa na mechi nyingine katika nchi mbalimbali zinazosaka kufuzu kwa fainali hiyo za 2013 nchi Afrika Kusini.Ethiopia watakuwa wenyeji Benin, huku Rwanda wakipepetana na Nigeria nayo Congo itaikaribisha Uganda wakati Burundi wataijaribu Zimbabwe mpya baada ya kuvunjwa kwa timu hiyo kutokana kashfa ya kupanga matokeo.

Jijini Nairobi wenyeji Kenya watakuwa na kibarua mbele Togo, wakati Gambia itaijaribu Algeria, huku Guinea Bissau itawavaa Cameroon, Tchad dhidi ya Malawi nayo Madagascar itaijaribu Cap Vert wakati Namibia itapepetana na Liberia. Chanzo, gazeti la Mwananchi

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.