LEO MAMBO MOTO BUNGENI`

WABUNGE WALIPUANA, BAADHI WATUHUMIWA KUUNGA MKONO UFISADI TANESCO, WIZARA YA NISHATI
Kizitto Noya, Dodoma
MOTO unatarajiwa kuwaka leo na kesho bungeni wakati wabunge watakapojadili bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baada ya kubainika njama za kutaka kuikwamisha bajeti hiyo ili kulinda watuhumiwa wa ufisadi.Kwa kipindi cha wiki moja sasa, kumekuwa na mpango unaoratibiwa na baadhi ya wabunge wakiwamo wa CCM na upinzani wanaotaka Waziri Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi wawajibishwe.

Muhongo na Maswi wanatuhumiwa kuwa, waliingilia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kuipa zabuni ya kununua mafuta Kampuni ya Puma Energy kinyume cha sheria ya ununuzi.

Katika sakata hilo, jana wabunge wa NCCR-Mageuzi waliamua kulipua mpango huo wakisema wamebaini njama za kutaka kukwamisha bajeti ya wizara na kutetea mafisadi ndani ya Tanesco na wizara ambao wamekuwa wakivuruga mfumo wa uzalishaji na usambazaji umeme nchini.

Msimamo wa NCCR Mageuzi ulikuja wakati ambao wabunge wa CCM walikuwa tayari wameupiga teke mpango wa wenzao wachache uliokuwa ukishinikiza kuwaondoa madarakani Muhongo na Maswi.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa chama hicho tawala zilisema kuwa, wabunge wengi walikuwa na msimamo mkali kwamba Maswi na Muhongo walipaswa kupongezwa hivyo kuweka kando hata jitihada za kukwamisha bajeti ya wizara hiyo.

NCCR Mageuzi
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Dodoma kwamba, taarifa za uhakika zimeonyesha kuwa mgawo wa umeme unaoonekana ukiendelea nchini una mkono wa baadhi ya wabunge na watendaji wa Tanesco, ambao wasingependa wanyang'anywe ulaji wao.

Mbatia alitangaza msimamo wa chama hicho akisema hakitakubali mpango huo ufanikiwe, kwani kimegundua kuwa ufisadi unaoitikisa wizara hiyo ikiwamo mgawo wa umeme ndani ya Tanesco una mkono wa baadhi ya wabunge.

Mbali na mgawo wa umeme, Mbatia alihoji wanaomtetea Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando baada ya kueleza kuwa, alishindwa kutatua mgawo wa umeme huku pia kitumia madaraka yake vibaya.

Alifafanua kwamba, ameona haja ya kutoa taarifa hiyo ili kueleza kutoridhishwa kwake na kampeni zinazoendelea miongoni mwa wabunge kutaka kuwasafisha baadhi ya wahusika wanaoendelea kulihujumu Shirika la Tanesco.

"Hapa bungeni kuna kampeni chafu zinaendelea ili kukwamisha bajeti na kutaka kusafishana. Lakini sisi NCCR Mageuzi tumeamua kuweka wazi hilo na kuwataka wabunge wafanye kazi zilizowaleta bungeni badala ya kuwasafisha watu kwa maslahi yao binafsi," alisema Mbatia na kuongeza:

"Mbunge ana kazi nne kimsingi, ambazo ni wajibu kwa taifa, wajibu kwa jimbo, wajibu kwa chama na wajibu kwa nafsi yake, lakini kutokana na baadhi yao kujihusisha na masuala ya uhujumu uchumi, wameamua kuyabadilisha majukumu hayo na kufanya wajibu kwa nafsi kuwa jukumu la kwanza."

Mbatia alisema baadhi ya wabunge wanashirikiana na baadhi ya watendaji katika wizara ya nishati na madini kulihujumu Taifa na wao kutumia nafasi walizonazo kuwatetea watendaji hao, kitu ambacho si jukumu la wawakilishi hao wa wananchi.

Akiwa na mkataba ambao Tanesco iliingia na Kampuni ya Santa Clara Supplies Limited kwa ajili ya usambazaji wa vifaa vya vifaa mbalimbali vya ofisa, Mbatia alisema kampuni hiyo inamilikiwa na mmoja wa vigogo wa shirika hilo akishirikiana na mkewe.

"Kwa maana nyingine, mkataba huu umeingiwa kitandani. Ndiyo namna watu wanavyojinufaisha na rasimali za nchi hii, lakini baadhi ya wabunge wanawatetea," alisema Mbatia aliyeongozana kwenye mkutano huo na wabunge wengine, Moses Machali, David Kafulila, Felix Mkosamali na Agripina Buyogela.

Mbatia alisema wakati kampuni hiyo inaanzishwa, mke wa kigogo huyo wa Tanesco alikuwa mfanyakazi wa shirika hilo kitengo cha stoo, lakini baada ya kuanza kupata zabuni hizo akaamua kuacha kazi ili aendelee kuisimamia kampuni hiyo akiwa nje.

Puma Energy
Katika hatua nyingine, Mbatia alionyesha kushangazwa na watu wanaobeza hatua iliyochukuliwa na Maswi kuipa zabuni Puma Energy ya kusambaza mafuta ya uzalishaji umeme kwa Tanesco na IPTL na kuziacha kampuni nyingine zilizokuwa na bei kubwa, akisema, hawana uzalendo.

“Hawa ndio majambazi na wahujumu uchumi tunaowasema. Kwa nini upinge uamuzi ambao unalifanya taifa liokoe Sh3 bilioni kila juma fedha ambayo siku zote ilikuwa inaingia kwenye mikono ya wajanja?," alihoji na kuendelea:

"Tunatoa wito kwa vyombo vya dola, vichunguze kuna nini hapa na wote watakaopatikana wanalihujumu taifa wachukuliwe hatua bila kujali nyadhifa zao,” alisema.

Wabunge wa CCM
Wakati NCCR Mageuzi wakitoa kauli hiyo, uamuzi huo wa Maswi uliungwa mkono pia katika mkutano wa ndani wa CCM uliofanyika juzi usiku, huku baadhi ya wabunge wakisema matatizo katika Sheria ya ununuzi, ndiyo yanayoliingiza taifa hasara.

Mkutano huo ulitanguliwa na vikao viwili vilivyokuwa na sura ya usuluhishi ambavyo chanzo chetu kilisema kuwa, viliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda vikiwashirikisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambao ni wabunge wa CCM pekee.

Vikao hivyo vilifanyika Jumanne na Jumatano mchana kabla ya kikao cha wabunge wa chama kilichofanyika siku hiyo usiku na kuongozwa na Pinda.

Mmoja wa wabunge wa CCM alisema jana kuwa: "Kama Maswi asingekuwa makini, hii ilikuwa Richmond nyingine. Tatizo sio viongozi, ni sheria zinazotawala manunuzi ya umma. Lowassa alijiuzulu kwa makosa ya namna hiyo".

Mbunge mwingine wa CCM, alisema Sheria za ununuzi wa umma zinapaswa kuangaliwa upya, kwani zina kasoro kubwa zinazotoa fursa kwa watu wasiokuwa waaminifu kulihujumu taifa. Chanzo; Mwananchi

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.