Mabosi wa mv Skagit waburuzwa kizimbani



HATIMAYE watendaji watatu wa Kampuni ya Seagull, ambayo inamiliki meli iliyozama ya mv Skagit iliyopinduka wiki iliyopita na kuua watu zaidi ya 80 visiwani Zanzibar wamefikishwa katika Mahakama ya Vuga mjini Zanzibar wakikabiliwa na tuhuma za mauaji ya bila kukusudia.

Akiwasomea shitaka hilo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Suleiman Masoud, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mussa Makame Musa, mkazi wa Kazole (nahodha wa meli), Saidi Abdulrhman Juma (mkurugenzi wa kampuni) na Omar Hasan Mkonje (meneja), mkaazi wa Magomeni.

Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa la mauaji bila ya kukusudia, jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 195 na 198 cha sheria namba 6 ya mwaka 2004, sheria namba 6 ya Serikali ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashitaka hayo yaliyosomwa na Suleiman Massoud Juma, washitakiwa hao wakiwa na dhamana na majukumu ya kuchukua abiria na mizigo yao, kwa uzembe walishindwa kuchukua tahadhari katika majukumu yao pasipo kuzingatia usalama wa tahadhari kwa abiria na kusababisha meli hiyo kuzama na kuua.

Inadaiwa kuwa Juni 18, mwaka huu, majira ya saa 7:30 mchana, washitakiwa wakiwa na dhamana ya kuchukua abiria na mizigo walishindwa kubeba majukumu yao pasipo kuzingatia usalama unaotakiwa, hivyo kusababisha meli hiyo kuzama baharini huko Chumbe.

Mawakili wa upande wa utetezi, Abdalla Juma na Rajab Abdalla, waliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wao kwa madai kuwa mashitaka yanayowakabili si miongoni mwa makosa yasiyopaswa kupatiwa dhamana.
“Mahakama kwa kuwa inao uwezo wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa, naomba wapewe dhamana kwa masharti nafuu watakayoweza kuyatimiza,” aliomba wakili Abdalla.

Wakili huyo alidai makosa yanayopaswa kunyimwa dhamana ni kuua kwa makusudi, kutumia silaha, kukutwa na dawa za kulevya na uhaini, lakini wateja wake hawakabiliwi na aina hiyo ya makosa.

“Suala hili liko ndani ya mamlaka yako katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la 10, imeweka wazi kwenye kifungu cha 12.1 kwamba watu wote ni sawa mbele ya sheria, wanayo haki ya kulindwa, mahakama ikiamua kuwapeleka ndani si sawa, ni kuwahukumu kwa kosa ambalo hawajalifanya,” alisema.

Baada ya utetezi huo, mahakama chini ya usimamizi wa Naibu Mrajis, Ali Ameir Haji, ilikubali hoja za mawakili wa washitakiwa na ikatoa dhamana kwa masharti ya kila mtuhumiwa kulipa fedha taslimu sh milioni tano pamoja na kudhaminiwa na wadhamini wawili.

Upande wa mashitaka umedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7, mwaka huu.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.