MKURUGENZI WA MAKUMBUSHO YA TAIFA ASIMAMISHWA KAZI

MKURUGENZI wa Makumbusho ya Taifa, Jackson Kihiyo amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi huyo alisema aliitwa na mkubwa wake wa kazi, ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na kufahamishwa kuwa amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwani kuna tuhuma kuhusu utendaji wake katika ofisi hiyo.

“Baada ya kupewa taarifa hizo, juzi(jumanne) nilikabidhi ofisi na hivi sasa nipo nyumbani. Cha muhimu ni kuwa sijafukuzwa ila nimesimamishwa na ninaendelea kupata mshahara wangu kama kawaida haid pale watakapomaliza huo uchunguzi wao,” alisema Kihiyo
Kihiyo alisema, hakutaka kumhoji mkuu wake wa kazi kuhusu tuhuma zinazomkabili kwa sababu alitaka wawe huru na wafuatilie kwa kina bila kuingiliwa, hivyo hadi sasa hafahamu kilichomsimamisha kazi.

“Najua wakimaliza watanijulisha, sina mashaka yeyote kwa sababu najua hakuna kibaya nilichofanya, nikiwauliza uliza watadhani ninataka kuwaingilia katika uchunguzi wao. Waache wafanye uchunguzi kwa utaratibu na kwa uhuru wakimaliza watanieleza kilichopatikana,” alisema Mkurugenzi huyo.

Chanzo cha habari kutoka katika ofisi hiyo kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake kilibainisha kuwa mkurugenzi huyo amefukuzwa baada ya wafanyakazi kupeleka malalamiko kwa katibu mkuu, Maimuna Tarishi, ikiwemo utata katika ukusanyaji wa mapato na maslahi ya wafanyakazi.

“Mkurugenzi alitoa amri ya kukusanya mapato katika vituo vyote na kisha mapato hayo katika akaunti ya makao makuu. Hili jambo lilizua maswali kwa sababu tutapelekaje mapato yote makao makuu, vituo vitajiendesha na nini? Lakini lingine ni maslahi duni ya wafanyakazi, hatujaboreshewa mishahara kwa muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa malalamiko mengine kuhusu utendaji wa mkurugenzi huyo ni kitendo cha Ofisi kutumia Menejimeti ya Umma kumuadhibu mfanyakazi badala ya kutumia Kamati ya Nidhamu jambo alilodai linasababisha uonevu mkubwa kwa wafanyakazi.

Shutuma nyingine dhidi ya Kihiyo ni upandishwaji wa vyeo kwa wafanyakazi usiozingatia sifa stahiki na kutokuwepo mipango endelevu ya mafunzo kwa wafanyakazi.

Kabla ya Kihiyo kushika nafasi hiyo, Mkurugenzi wa Makumbusho alikuwa ni Nobert Kayombo, ambaye alifariki Novemba 30, 2010.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.

DK NCHIMBI ATINGA MKOANI KATAVI