MMILIKI WA MELI, YA SKAGIT NAHODHA WATIWA MBARONI



JESHI la Polisi Zanzibar linawashikilia wafanyakazi sita wa meli ya MV Skagit akiwemo mmiliki wake Saidi Abdulrahman pamoja na nahodha wa meli hiyo, Mussa Makame Mussa, wanahojiwa na polisi.

Watuhumiwa hao walikuwa wakihojiwa katika Ofisi za Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi mjini Zanzibar ambapo Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuph Ilembo, amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Kamanda Ilembo amesema kuwa makachero wa polisi wanaendelea na uchunguzi na kutafuta taarifa nyingine zinazohusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, nahodha wa zamu siku ya tukio hilo la kupinduka na kuzama kwa meli hiyo ya MV Skagit, Mussa Makame Mussa, ameelezea kwa ufupi jinsi ajali hiyo ilivyotokea na namna yeye alivyonusurika.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya kupigwa na dhoruba na mawimbi yaliyoambatana na upepo mkali, ambapo yeye alinusurika kufa maji baada ya kuruka kwa kutumia mlango wa mbele wa meli hiyo na kuanza kuogelea ambapo alijichanganya pamoja na abiria wengine walionusurika na kuokolewa na vyombo vya uokozi.

Wakati huohuo, wapiga mbizi wa vikosi vya ulinzi na usalama leo wamefanikiwa kuzipata maiti nyingine tano akiwemo mwanamke mmoja na wanaume wanne.
Katika upekuzi wa maiti hizo, makachero wa polisi walibaini kitambulicho cha kupigia kura kutoka kwa mmoja wa marehemu kilichokuwa na jina la Philip John Busiya aliyezaliwa mwaka 1977 katika kijiji cha Mapilinga, kata ya Igokelo, wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

Kupatikana kwa miili hiyo, kunaifanya idadi ya maiti kufikia 73. Maiti nyingine 68 zilipatikana siku za mwanzo baada ya kutokea kwa ajali hiyo ambapo kati ya hizo, maiti 54 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.

Maiti hiyo iliyopewa namba 72, pamoja na maiti nyingine nne, zimezikwa katika makaburi ya pamoja ya Kama yaliyoko nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Eneo hilo la Kama pia lilitumika kwa kuwazika watu wengine waliokosa ndugu wakati wa ajali ya meli ya Spice Islander iliyotokea Septemba 9, 2011.

Kupatikana kwa miili hiyo kumetokana na juhudi zinazoendelea kwa kuvishirikisha vikosi vya ulinzi na usalama, wazamiaji wa makampuni binafsi pamoja na Mamlaka ya Bandari Zanzibar wakati wakiwa katika harakati za kuitafuta boti hiyo ili kuweza kubaini kama kuna miili mingine iliyosalia kwenye meli hiyo chini ya bahari.

Aidha, juhudi za kutaka kuiibua meli hiyo zinaendelea ambapo wazamiaji wa JWTZ, polisi, KMKM, JKU, Bandari na wale wa makampuni binafsi na wale wa kujitegemea wakiendelea na kazi ya kutafuta mahali ilipo meli hiyo ili kuona kama wataweza kupata miili mingine iliyonasa kwenye vyumba vya meli hiyo ambayo imekokotwa na maji kutoka eneo ilipozama.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.